Rais William Ruto aapa kumzima Raila Odinga daima dawamu

Ruto aliyemtaja Raila kama ‘Mfalme wa Machafuko’ alishangaa ni watu wangapi zaidi wangekufa kabla ya kusitisha maandamano hayo.

Muhtasari

• "Raila anapaswa kufahamu kuwa uchaguzi ulimalizika mwaka jana na hatutaruhusu njia zozote za mkato nje ya katiba kujiunga na serikali," alisema. 

Kinara wa upinzani Raila Odinga na Rais William Ruto.
Kinara wa upinzani Raila Odinga na Rais William Ruto.
Image: FILE

Rais William Ruto ameapa kuwa serikali itafanya kila iwezalo kukomesha maandamano ya ghasia ambayo yamesababisha vifo vya watu wengi na mali ya mamilioni kuharibiwa. 

Ruto alisema kuwa yeye binafsi atakabiliana na maandamano ambayo yameitishwa na upinzani kupinga kupanda kwa gharama ya maisha. Bila kueleza atachukua hatua gani, Ruto alisema kuwa atamdhibiti kiongozi wa upinzani Raila Odinga daima dawamu.

 "Kuanzia sasa na kuendelea hakutakuwa na maandamano tena na yeyote aliye tayari kufanya maandamano atafanya hivyo kutoka kwa nyumba yake," Rais alisema. 

Haya yalijiri saa chache baada ya muungano wa Azimio La Umoja kutangaza kuwa wiki ijayo maandamano hayo yataendeshwa kwa siku tatu kuanzia Jumatano hadi Ijumaa. Akijibu haya, Ruto alimshutumu Raila kwa kuendelea kupoteza maisha na mali na kuongeza kuwa wakati ulikuwa umefika wa kumdhibiti yeye na wandani wake. 

Akizungumza katika kituo cha Kinamba mjini Naivasha baada ya kufungua rasmi barabara ya Naivasha-Njabini, Rais alikiri kwamba gharama ya maisha imepanda. 

"Katika miezi ijayo tutakuwa na mavuno mengi nchini kote kufuatia mpango wetu wa ruzuku ya mbolea na hii itapunguza gharama ya maisha," alisema. 

Alikuwa mwepesi kutambua kuwa gharama ya maisha haitashughulikiwa kupitia maandamano ya ghasia huku akipuuza ‘handshake’ na Raila. 

"Raila anapaswa kufahamu kuwa uchaguzi ulimalizika mwaka jana na hatutaruhusu njia zozote za mkato nje ya katiba kujiunga na serikali," alisema. 

Ruto aliyemtaja Raila kama ‘Mfalme wa Machafuko’ alishangaa ni watu wangapi zaidi wangekufa kwa kisingizio cha maandamano kabla ya kusitisha maandamano hayo. 

"Ndugu wa handshake wanalipa vijana kusababisha machafuko nchini na ilhali wao ndio wanahusika wakuu wa kuzorota kwa uchumi baada ya kuachia taifa deni la Shilingi trilioni 9," alisema.