Maandamano yataisha tu wakati Ruto atakapobatilisha Sheria ya Fedha - Sifuna

Akizungumza mjini Kibra siku ya Jumatano, ambapo aliwaongoza wafuasi wa Azimio katika maandamano hayo

Muhtasari
  • Aliwashukuru maaskofu wa Kanisa Katoliki kwa kumtaka Ruto kubatilisha Sheria hiyo akisema itawaelemea Wakenya iwapo itatekelezwa.
b6251efb2cdb00bc
b6251efb2cdb00bc

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ameshikilia kuwa maandamano ya upinzani dhidi ya serikali yatakoma tu wakati Rais William Ruto atakapobatilisha Sheria ya Fedha, 2023.

Akizungumza mjini Kibra siku ya Jumatano, ambapo aliwaongoza wafuasi wa Azimio katika maandamano hayo, Sifuna alisema maandamano hayamhusu kiongozi wa Upinzani Raila Odinga bali gharama ya juu ya maisha.

Aliwashukuru maaskofu wa Kanisa Katoliki kwa kumtaka Ruto kubatilisha Sheria hiyo akisema itawaelemea Wakenya iwapo itatekelezwa.

“Tunataka kumwambia Rais William Ruto kwamba ikiwa hatabatilisha Sheria ya Fedha, 2023, watu hawataondoka barabarani,” akasema.

Aidha aliikashifu serikali kwa kuwakamata viongozi wa Azimio bila sababu.

"Tunapozungumza, bado hatuelewi alipo Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino," alisema.

Aliitaka serikali kukomesha kile alichokitaja kuwa matumizi ya kuchagua ya polisi.

Matamshi yake yanajiri muda mfupi baada ya maaskofu wa katoliki kumtaka Ruto kubatilisha sheria hiyo.

Viongozi hao wamewataka viongozi wa pande mbili kusikiliza na kuzingatia maslahi ya wananchi na kuhakikisha amani inapatikana kwa njia ya amani.

Aidha wamewataka polisi kulinda usalama wa raia badala ya kutumia nguvu kupita kiasi na kusababisha vifo dhidi ya raia.

Viongozi hao pia walitangaza mipango ya kuitisha mazungumzo ya kitaifa huku wakiwataka Wakenya kupinga uchochezi na kuchochewa vurugu.