Maandamano: Tunachofahamu kufikia sasa kuhusu maandamano Kenya

Mashirika mawili tofauti ya haki za binadamu yametaja idadi ya waliofariki katika maandamano nchini Kenya kufikia watu 30

Muhtasari

• Mashirika ya haki za kibinadamu yaonya dhidi ya utumizi wa nguvu kupitia kiasi.

 

Polisi wakikabiliana na waandamanaji nchini Kenya.
Polisi wakikabiliana na waandamanaji nchini Kenya.
Image: BBC

Tukianzia katika kaunti ya Kisumu ni kwamba baada ya hali mbaya ya mshikemshike kati ya waandamanaji na polisi hapo jana , hii leo hali imekuwa tulivu ijapokuwa biashara zimefungwa na hakuna kinachoendelea kwasababu mji umesalia kuwa mahame ijapokuwa idadi ya maafisa wa polisi imeongezeka katika mji huo .

Vilevile katika mkoa wa kati kulikuwa na hali tete katika kituo cha polisi cha Wanguru huko Mwea baada ya jamaa na familia ya mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kufika katika kituo hicho wakitaka kiongozi huyo aliyekamatwa hapo jana kuachiliwa la sivyo awasilishwe mahakamani.`Hatahivyo mbunge huyo alidaiwa kuondolewa katika kituo hicho na duru zimearifu kwamba amehamishwa katika kituo kimoja cha polisi mjini Nairobi.

Katika eneo la Saboti kituo cha biashara cha Matisi , mtu mmoja amedaiwa kudungwa kisu hadi kufa alipokuwa akijaribu kuzima moto uliokuwa umewashwa na waandamanaji.

Mashirika ya haki za kibinadamu yaonya dhidi ya utumizi wa nguvu kupitia kiasi


Waandamanaji Kenya
Waandamanaji Kenya
Image: BBC

Wakati huohuo mashirika mawili tofauti ya haki za binadamu yametaja idadi ya waliofariki katika maandamano nchini Kenya kufikia watu 30 tangu maandamano ya kuipinga serikali yaanze wiki mbili zilizopita.

Shirika la Amnesty International kupitia Mkurungenzi wake Mkuu Irungu Houghton wakati huohuo limeshtumu utumiaji wa nguvu kupitia kiasi unaotekelezwa na maafisa wa polisi dhidi ya waandamanaji.

Vilevile shirika la haki zi kibinadamu la Haki Afrika limewataka maafisa wa polisi kutotumia kile walichokitaja kuwa nguvu kupitia kiasi dhidi ya waandamanaji wanaopigania haki yao.

Kiongozi wa shirika hilo Hussein Khalid amesema kwamba takriban watu 27 wameripotiwa kufariki tangu maandamano hayo ya kuipinga serikali yalipoaza wiki mbili zilizoisha kutokana na nguvu za kupitia kiasi zinazotumiwa na maafisa wa polisi.

Hivyobasi Shirika hilo limetoa wito kwa vinara wawili Rais William Ruto na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kulegeza misimamo yao na kuendelea na majadiliano ili kutafuta suluhu ya mambo yanayowakumba Wakenya kwa sasa.

Wamesema kwamba asilimia kubwa ya wanaoathirika ni Watoto na wanawake huku wakitaka hali hiyo itatuliwe kwa haraka.

Polisi wakabiliana na waandamanaji Kibra

Vilevile katika eneo la Kibra ambalo lipo jijini Nairobi,

Ghasia zinaendelea kuripotiwa huku polisi wakikabliana na baadhi ya waandamanaji katika mtaa wa `Woodely.

Tukisalia jijini Nairobi katika eneo la Mathare: Maafisa wa usalama wanazidi kuwazuia waandamanaji hususan katika eneo la number 10. Moshi mweusi umetanda katika eneo hilo kutokana na vitoa machozi. `Polisi wanaendelea kuwazuia waandamanaji na kuwarudisha hadi katika makazi yao.

Katika eneo la Kangemi lililoshuhudia hali mbaya ya maandamano siku ya Jumatano utulivu mdogo umerejea ijapokuwa kuna idadi kubwa ya polisi. Matairi yaliokuwa yamewashwa moto hapo jana yamekuwa yakiendelea kuondolewa katika baadhi ya barabara. Baadhi ya raia wamefungua biashara zao huku usafiri ukiendelea kama kawaida.