Mbunge wa Embakasi Masihariki Babu Owino aachiliwa kwa dhamana

Pia walioachiliwa kwa bondi ni rais wa Ghetto Gaucho, Tom Odondo, Michael Otieno, Pascal Ouma, Kevin Wambo na Willys Owino.

Muhtasari

• Siku  ya Alhamisi, Babu Owino na Gaucho walikanusha njama ya kutekeleza shughuli za uasi ambazo zinaathiri utulivu wa umma.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na rais wa Ghetto Calvin Gaucho wameachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Shilingi 100,000 kila mmoja.

Hakimu mkuu wa Milimani Lukas Onyina katika uamuzi wake Ijumaa asubuhi alibainisha kuwa shtaka dhidi ya washtakiwa linaweza kuadhibiwa wakipatikana na hatia kwa kifungo cha miaka saba gerezani.

Onyina aliongeza kuwa moja ya sababu zilizotolewa na upande wa mashtaka ni kwamba washtakiwa walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuingilia mashahidi.

Hata hivyo, alisema upande wa mashtaka haujabainisha ni nani kati ya washtakiwa hao ataingilia mashahidi.

"Uchunguzi kamili wa hati ya kiapo hauonyeshi sababu za msingi za kuwanyima dhamana washtakiwa. Kila mmoja wa washtakiwa anapewa bondi ya Sh200,000 na dhamana ya fedha taslimu Shilingi 100,000," aliamuru hakimu.

Pia walioachiliwa kwa bondi ni Tom Odondo, Michael Otieno, Pascal Ouma, Kevin Wambo na Willys Owino.

Siku  ya Alhamisi, Babu Owino na Gaucho walikanusha njama ya kutekeleza shughuli za uasi ambazo zinaathiri utulivu wa umma.

Inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya Julai 7 na 23, 2023 na wengine ambao hawakufikishwa mahakamani katika Kaunti ya Jiji la Nairobi.

Upande wa mashtaka ulikuwa umepinga kuachiliwa kwao kwa dhamana ukieleza kuwa kuna vipengele vingine vya uchunguzi ambavyo bado vinaendelea na ambavyo vitaathiri iwapo wataachiliwa kwa dhamana.

Wakili wa upande wa mashtaka aliitaka mahakama kuwa radhi kuwanyima dhamana kila mshtakiwa na kuwazuilia washukiwa hao hadi upelelezi ukamilike. Mahakama iliambiwa kuwa washtakiwa hao walikuwa tishio kwa usalama wa taifa.

"Katika tarehe kati ya tarehe 7 Julai 2023 na 18 Julai 2023, watu wanaoaminika kuwa washirika wa washtakiwa walikusanyika kinyume cha sheria na kuzua ghasia katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Nairobi na hivyo kufanya makosa kadhaa ya adhabu kama walivyoshtakiwa katika mashtaka," DPP aliwasilisha.

DPP alidai kuwa pia kuna uwezekano wa mashtaka ya ziada kupendekezwa dhidi ya kila mmoja wa Walalamikiwa baada ya upelelezi unaoendelea kukamilika.

Upande wa utetezi kupitia kwa mawakili Danstan Omari, Dancun Okatch, Ndegwa Njiru miongoni mwa wengine waliambia mahakama kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa na upande wa mashtaka ya kuwanyima washtakiwa dhamana ni sawa na ile iliyotumika kuanzia 2017 hadi 2022 kuwakandamiza wananchi.