Familia ya Uhuru yaamriwa kusalimisha bunduki zote walizo nazo

Familia hiyo inatarajiwa kusalimisha silaha 28 zilizosajiliwa kwa majina yao kwa Bodi ya Leseni za Silaha jijini Nairobi.

Muhtasari

•Serikali imeiamuru familia ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kusalimisha bunduki zote walizonazo.

•Uhuru aliapa kutetea familia yake dhidi ya mashambulizi yoyote.

Image: Maktaba

Serikali imeiamuru familia ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kusalimisha bunduki zote walizonazo.

Familia hiyo inatarajiwa kusalimisha silaha 28 zilizosajiliwa kwa majina yao kwa Bodi ya Leseni za Silaha jijini Nairobi.

Katika video iliyofikia Radio Jambo, afisa wa polisi anasikika akieleza kuwa alitumwa na mwenyekiti wa Bodi ya Leseni ya Silaha Yakub Rashid.

Haya yanajiri baada ya rais huyo wa zamani kudai kuwa polisi walivamia nyumba ya mwanawe Jomo Kenyatta katika mtaa wa Karen ili kufanya msako wa kutafuta silaha.

Uhuru aliapa kutetea familia yake dhidi ya mashambulizi yoyote.

Aliambia serikali kukabiliana naye ana kwa ana badala ya kuifuata familia yake.

"Ukweli kwamba nimekuwa kimya haimaanishi kuwa nina hofu. Njoo kwangu ikiwa ni mimi unayetaka," Uhuru alisema.

"Nilifanya kadri nilivyoweza kuifanyia nchi yangu na nilikabidhiana mamlaka wakati muda wangu ulipokwisha na sasa nitafanya kila liwezekanalo kuitetea familia yangu."

Rais huyo wa zamani alitoa wito kwa serikali kusuluhisha tofauti zozote za kisiasa na yeye pekee, badala ya kuwaingilia wanafamilia wake wa karibu.

"Ombi langu pekee ni kwamba usipangie mama yangu au watoto wangu. Nipangie mimi ndiye unayetaka. Wanahusika vipi na chochote," alisema.

Uhuru aliongeza kuwa watu wengi nchini Kenya wana leseni ya kubeba silaha na walifuata taratibu zinazofaa kuzipata.

Siku ya Ijumaa, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema bunduki 23 zilipatikana kutoka kwa nyumba tatu katika mtaa wa Karen, Nairobi, kufuatia operesheni iliyoanzishwa baada ya kubainika kuwa silaha zilizotumiwa wakati wa maandamano zilitolewa na watu waliokuwa na bunduki za kiraia.

"Leo alasiri, operesheni imekuwa ikiendelea kulenga nyumba tatu ndani ya eneo la Karen ambapo jumla ya bunduki 23, ambazo baadhi yao zinashukiwa kutumika katika shughuli haramu zimehifadhiwa," alisema.