Mjakazi anayeshukiwa kumuua afisa wa Kilifi akamatwa Kakamega

Mshukiwa alikuwa amewaambia baadhi ya marafiki zake kwamba alikusudia kuondoka kwenda Uganda kwa muda.

Muhtasari

•Mshukiwa alikuwa amewaambia baadhi ya marafiki zake kwamba alikusudia kuondoka kwenda Uganda kwa muda.

•Wapelelezi wa polisi wanasema mshukiwa alimdunga kisu mwajiri wake baada ya mabishano kuhusu pesa.

Marehemu Rahab Karisa
Image: HISANI

Mjakazi anayeshukiwa kumuua Afisa Mkuu wa Uvuvi na Uchumi wa Maji katika kaunti ya Kilifi Rahab Karisa amekamatwa.

Polisi walisema alikamatwa Kakamega alipokuwa akijaribu kutorokea Uganda.

Mwanamke huyo anatoka Bungoma na alikuwa amewaambia baadhi ya marafiki zake kwamba alikusudia kuondoka kwenda Uganda kwa muda.

Maafisa wa upelelezi walisema alifuatwa hadi Kakamega ambako alikuwa akitafuta mwelekeo wa kuelekea alikokuwa akienda.

Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika eneo la Pwani, Ali Bule alithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa.

"Alikamatwa Kakamega na timu iko njiani kuja naye," alisema.

Wapelelezi wa polisi wanasema mshukiwa alimdunga kisu mwajiri wake baada ya mabishano kuhusu pesa.

Rahab alikuwa amewasili tu kutoka kwa ziara ya kikazi ya juma moja nchini Italia wakati mabishano yalipotokea kati yake na shangazi yake, na msaidizi wa nyumbani.

Wachunguzi walisema kuwa Rahab alipata Sh32,000 zikiwa hazipo kati ya Sh100,000 alizokuwa akihifadhi nyumbani kwake.

"Alitafuta majibu kutoka kwa mjakazi pamoja na shangazi yake kuhusu mahali zilipo pesa na kutishia kuwaripoti kwa polisi asubuhi," mpelelezi alisema.

Matokeo ya awali yanaonyesha kwamba alimuuliza kijakazi ambaye aliokota pesa hizo na akakanusha kujua.

Hili liligeuka kuwa kelele na kusababisha mapigano ambayo yalimwacha afisa huyo na majeraha ya kisu. Alitokwa na damu hadi kufa nyumbani kwake.

Jirani yao mmoja alisema walisikia mtu akipiga kelele mara moja lakini hakuna aliyefikiria sana hadi walipoanza kusikia zogo katika boma hilo.

Watoto wake walikuwa kwenye chumba tofauti bila kufahamu mkasa huo. Polisi wanasema angeweza kunusurika kama angepata usaidizi.

"Alikufa kwa kutokwa na damu. Angepata msaada angekuwa hai,” afisa mmoja alisema.