Gavana Nyong'o alipa bili za hospitali za waathiriwa wa maandamano

Gavana Anyang' Nyong'o alifichua kuwa zaidi ya wakazi 100 wa Kisumu walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.

Muhtasari
  • Gavana Nyong'o alisikitika kwamba zaidi ya wakazi 90 wa Kisumu walitendewa kinyama na polisi na kulazimika kulazwa kwa muda mrefu.
  • Tangazo la Gavana Nyongo lilijiri hata wakati upinzani ulifanya mikesha kote nchini kwa heshima ya Wakenya waliopoteza maisha wakati wa maandamano hayo.
Gavana Nyong'o alipa bili za hospitali za waathiriwa wa maandamano
Image: TWITTER

Serikali ya Kaunti ya Kisumu mnamo Jumatano, Julai 26, ililipa bili zote za hospitali na chumba cha kuhifadhi maiti kwa kila mtu aliyejeruhiwa au kuuawa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali yaliyoandaliwa na muungano wa Azimio.

Katika taarifa iliyosomwa na Spika wa Kaunti ya Kisumu, Elisha Oraro, Gavana Anyang' Nyong'o alifichua kuwa zaidi ya wakazi 100 wa Kisumu walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.

Gavana Nyong'o alisikitika kwamba zaidi ya wakazi 90 wa Kisumu walitendewa kinyama na polisi na kulazimika kulazwa kwa muda mrefu.

Spika Oraro alisoma taarifa yake nje ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga ambapo wakazi wa Kisumu walifanya mkesha kwa heshima ya Wakenya waliopoteza maisha wakati wa maandamano hayo.

Kauli ya Gavana huyo pia ilidokeza kuwa uchunguzi kuhusu kiwango cha ukatili unaofanywa dhidi ya wakazi wa Kisumu unaendelea na wale wote watakaopatikana na hatia watafikishwa mahakamani.

Wakazi wa Kisumu walikaribisha msamaha wa gavana na kuendelea kuwasha mishumaa na kuombea roho za marehemu.

Tangazo la Gavana Nyongo lilijiri hata wakati upinzani ulifanya mikesha kote nchini kwa heshima ya Wakenya waliopoteza maisha wakati wa maandamano hayo.

Upinzani umekuwa ukifanya maandamano kote nchini kupinga masuala mbalimbali.