Maandamano dhidi ya gharama ya maisha kurejelewa Jumatano ijayo - Wandayi

Azimio itaanzisha hazina maalum ya wahanga wa ukatili wa polisi kuwalipa fidia waliopoteza mali wakati wa maandamano hayo.

Muhtasari

• Mbunge huyo ameelezea kusikitishwa na mwaliko wa Rais William Ruto kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kupitia ujumbe wa Twitter.

amekamatwa
Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi amekamatwa
Image: JACK OWUOR

Kiongozi wa walio wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi amesema watarejelea maandamano ya amani Jumatano wiki ijayo.

Wandayi siku ya Jumatano alisema walisitisha kwa muda maandamano hayo kwa heshima ya waathiriwa wa maandamano ya wiki jana.

Aidha ameeleza kuwa wataanzisha hazina maalum ya wahanga wa ukatili wa polisi itakayotumika kuwalipa fidia waliopoteza mali wakati wa maandamano hayo.

"Wiki hii ni maalum kwa maombi; tutakuwa na maombi ya madhehebu mbalimbali Nairobi, Kisumu na miji mikuu," alisema.

Wakati huo huo mbunge huyo ameelezea kusikitishwa na mwaliko wa Rais William Ruto kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kupitia ujumbe wa Twitter.

Rais Ruto alitumia mtandao wa Twitter siku ya Jumanne, akisema kwamba yuko tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na kinara wa upinzani mara tu atakaporejea kutoka Tanzania ambako anahudhuria mkutano wa rasilimali ya utendakazi.

"Rafiki yangu Raila Odinga, ninaenda Tanzania kwa mkutano wa rasilimali watu ili kuoanisha upanuzi wa nafasi za ajira katika bara letu," uisoma ujumbe wa Ruto.

Wandayi alikashifu mwaliko huo wa Ruto akisema sio ustaarabu kwa rais kumwalika kiongozi huyo wa upinzani kupitia taarifa kwenye mitandao ya kijamii.

"Ruto lazima amheshimu Baba, kumwalika kupitia tweet ni kukosa heshima," alisema Wandayi.

Kiongozi wa wachache ambaye pia ni mbunge wa Ugunja hata hivyo alisema muungano wa Azimio la Umoja uko tayari kufanya mazungumzo na serikali.