Serikali yatiwa breki! mahakama yasitisha hatua ya kumpokonya bunduki Jomo Kenyatta

Jomo Kenyatta alikuwa ameomba mahakama iingilie kati na kukomesha serikali kumpokonya leseni yake ya kumiliki bunduki.

Muhtasari

Jomo Kenyatta alikuwa ameomba mahakama iingilie kati na kukomesha serikali kumpokonya leseni yake ya kumiliki bunduki.

Rais Mustaafu Uhuru Kenyatta na mwanawe Jomo Kenyatta.
Rais Mustaafu Uhuru Kenyatta na mwanawe Jomo Kenyatta.
Image: HISANI

Mahakama kuu imesitisha uamuzi wa serikali wa kufutilia mbali leseni ya kumiliki silaha ya Jomo Kenyatta mwanawe rais Uhuru Kenyatta. 

Hapo awali, katika ombi la dharura mbele ya Mahakama ya Milimani, mwanawe Rais wa Zamani John  Jomo Kenyatta alikuwa ameomba mahakama iingilie kati na kukomesha serikali kumpokonya leseni yake ya kumiliki bunduki.

Mwanawe rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, John Jomo Kenyatta aliwasilisha kesi mahakama ya kuu kupinga uamuzi wa serikali kufutilia mbali leseni yake kumiliki bunduki.

Katika ombi la dharura mbele ya Mahakama ya Milimani, Jomo ameiomba mahakama kuingilia kati na kukomesha serikali kuzuiwa kutekeleza uamuzi wa kumpokonya leseni ya kumiliki silaha.

Jomo anamtaka afisa mkuu wa Bodi ya Leseni za silaha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusitisha ombi lake la kutaka kufutili mbali leseni yake ‘bila kufuata utaratibu uliowekwa katika Sheria ya Silaha’.

Katika barua yake kwa mahakama, kupitia kwa Wakili wake Fred Ngatia,  Jomo anasema uamuzi wa kunyang’anywa leseni yake ya kumiliki silaha ni kinyume na kifungu cha 5 (8) cha Sheria ya Silaha.

Anadai hajafahamishwa sababu za kufutiliwa mbali kwa leseni hiyo.

Jomo alisema maafisa walipokuja wakimtaka asalimishe bunduki zake Julai 21, hakuna sababu iliyotolewa.

"Nilipotaka kufahamu sababu kama zipo, zilizosababisha hatua hiyo ya ghafla, maafisa hao walijifanya kutojua," Jomo alisema.

Kulingana na hati za mahakama, leseni yake ni halali hadi Aprili 27, 2024.

Siku ya Ijumaa, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alidai kwa jumla ya bunduki 23 zilipatikana kutoka kwa nyumba tatu mtaani Karen, Nairobi, kufuatia operesheni iliyoanzishwa baada ya kubaini kuwa  baadhi ya silaha zilizotumiwa wakati wa maandamo zilitolewa na watu waliokuwa na bunduki za kiraia.