Mawaziri wafungiwa nje ya ikulu kwa kuchelewa, Ruto awaagiza kuandika barua ya maelezo

"Nitatarajia maelezo ya kibinafsi kuhusu ni kwa nini ulichelewa na usitumie trafiki kama kisingizio," Ruto alisema.

Muhtasari

•Ruto ambaye alijawa ghadhabu baada ya Waziri Kithure Kindiki na mwenzake Moses Kuria kufungiwa nje ya Ikulu kwa kuchelewa alisema anahitaji maelezo.

•Kulingana na ratiba rasmi iliyotolewa na Katibu wa Habari wa Ikulu Emmanuel Talam, hafla hiyo ilikuwa ianze saa mbili kamili asubuhi. 

Rais William Ruto
Image: PCS

Rais William Ruto amewataka mawaziri wawili waliokosa kutia saini kandarasi za utendakazi kwa kuchelewa kueleza sababu zao kwa maandishi.

Ruto ambaye alijawa ghadhabu baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na mwenzake wa Biashara Moses Kuria kufungiwa nje ya Ikulu kwa kuchelewa, alisema anahitaji maelezo.

"Sielewi ni kwa nini mtu anaweza kukosa hafla muhimu kama hii ambayo inahusisha kazi yake. Kwa wewe kukosa tukio kama hili, umejiondoa," Ruto alisema.

Rais alisema zaidi kwamba mawaziri waliofungiwa nje wanapaswa kumwandikia yeye binafsi kueleza kwa nini walichelewa.

"Nitatarajia maelezo ya kibinafsi kuhusu ni kwa nini ulichelewa na usitumie trafiki kama kisingizio," Ruto aliongeza.

Kulingana na ratiba rasmi iliyotolewa na Katibu wa Habari wa Ikulu Emmanuel Talam, hafla hiyo ilikuwa ianze saa mbili kamili asubuhi. Hii ilimaanisha kwamba mawaziri wote na Makatibu Wakuu wao walipaswa kuwa wameketi mapema vya kutosha kabla ya muda rasmi wa hafla hiyo kuanza.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Naibu Rais Rigathi Gachagua aliwaonya Mawaziri na Wabunge kuhusu kuchelewa akisema kwamba hakuwezi kuwa na sababu zozote za hilo.

“Niliona wengine wamechelewa, nikamtazama Rais machoni na kugundua kuwa kutakuwa na matatizo kwao,” Gachagua alisema.

"Huwezi kufika kwenye tukio wakati Rais tayari ameketi. Kwa nini uchelewe? Unaelezaje hilo? Ulikwenda kuonana na nani na bado leo ilikuwa siku muhimu kwako kusaini mikataba?"

Naibu Rais alitoa onyo hilo na kufichua kuwa hapo awali rais Ruto alikasirika aliposhindwa kufanya kikao cha Baraza la Mawaziri kutokana na utoro wa mawaziri zaidi ya saba.