IG Koome asema polisi hawatatishwa na vitisho kupelekwa ICC

Siku ya Jumanne, Koome alisema polisi wana mamlaka kisheria kuwalinda Wakenya na hawatakubali vitisho.

Muhtasari

• Akitetea vitendo vya polisi wakati wa maandamano, Koome alisema kuwa polisi wana jukumu la kulinda maisha na mali. 

IG Koome awaambia Azimo vitisho vya ICC haviwezi kumtisha
IG Koome awaambia Azimo vitisho vya ICC haviwezi kumtisha
Image: STAR

Inspekta Jenerali Japhet Koome amewajibu wakosoaji kuhusu vitisho vya kumpeleka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutokana na vifo vilivyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya mwezi uliopita. 

Siku ya Jumanne, Koome alisema polisi wana mamlaka kisheria kuwalinda Wakenya na hawatakubali vitisho. 

"Vichwa vya habari vya propaganda hazitatutisha. Wanaweza kuendelea kututishia kwenda mahakama ya ICC na hilo halina maana yoyote kwetu katika dhamira yetu ya kutumikia na kulinda nchi yetu," alisema. 

Akitetea vitendo vya polisi wakati wa maandamano, Koome alisema kuwa polisi wana jukumu la kulinda maisha na mali. 

"Ninataka kuwaambia Wakenya kwamba kama Huduma ya Kitaifa ya Polisi, tuna jukumu la kulinda maisha na mali. Tuna jukumu la kuhakikisha nchi yetu iko salama na ni jukumu ambalo tutatekeleza bila uoga wala upendeleo," aliongeza. 

Mwezi uliopita, muungano wa Azimio la Umoja uliitaka ICC kuingilia kati hali inayoendelea nchini. Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alikuwa ameitaka ICC kuchunguza maovu yaliotekelezwa na polisi.

 "Tumeona kiwango cha kusikitisha cha ukatili wa polisi kwa Wakenya wasio na hatia. Tunataka Jamii ya kimataifa kuzingatia kwa uzito matukio haya ili kuwatilia vikwazo wahusika wa mauaji hayo," alisema kisha.

"Tunaiomba ICC kuzingatia zaidi hali ya Kenya kwa sababu tunachoshuhudia ni uhalifu dhidi ya ubinadamu."