Mshukiwa mkuu katika mauaji ya afisa wa DCI Kayole akamatwa

Mshukiwa Alex Wanjiru, 23, alitolewa kutoka mafichoni mwake katika nyumba ya nyanyake huko Ruthingiti, Kaunti ya Kiambu.

Muhtasari

• Vikosi maalum vya polisi vinaendelea na msako mkali kuwatafuta washukiwa wengine wawili ambao bado hawajakamatwa.

Alex Wanjiru mshukiwa wa mauaji ya afisa wa DCI Konstebo David Mayaka aliyepigwa risasi mtaani Kyole.
Alex Wanjiru mshukiwa wa mauaji ya afisa wa DCI Konstebo David Mayaka aliyepigwa risasi mtaani Kyole.
Image: DCI

Mmoja wa washukiwa wakuu wa mauaji ya kutatanisha ya afisa wa DCI amekamatwa.

Picha za CCTV zilionyesha wauaji wakiendesha pikipiki, wakifyatua risasi na kumpiga risasi Konstebo David Mayaka tumboni, na mkewe Hellen Kemunto akipigwa risasi kwenye paja walipokuwa katika harakati za kubadilisha tairi la gari lao.

Idara ya DCI ilisema kwamba mshukiwa Alex Wanjiru, 23, alitolewa kutoka mafichoni mwake katika nyumba ya nyanyake huko Ruthingiti, Kaunti ya Kiambu, na pikipiki inayoaminiwa kutumika akitoroka ikanaswa.

Wanjiru alimkimbia mtaa wa Kayole mara tu baada ya kudaiwa kutekeleza uhalifu huo, kulingana na DCI, na alikamatwa kufuatia oparesheni ya pamoja iliyohusisha maafisa wa vitengo maalum vya ujasusi katika makao makuu ya DCI.

Pikipiki inayoamika kutumika wakati wa mauaji pia ilinasawa.
Pikipiki inayoamika kutumika wakati wa mauaji pia ilinasawa.
Image: DCI

 DCI pia ilibainisha kuwa ripoti ya kisayansi tangu wakati huo imehusisha bunduki iliyotumiwa katika uhalifu huo na matukio matano ya ujambazi jijini Nairobi.

Vikosi maalum vya polisi vinaendelea na msako mkali kuwatafuta washukiwa wengine wawili ambao bado hawajakamatwa.

"Kufikia sasa, maafisa wa upelelezi pia wamewatambua watu wengine wawili waliohusika katika mauaji hayo,” idara ya DCI ilisema.

Kulingana na ripoti ya awali ya uchunguzi Henry Njihia aliyefyatua risasi na kumuua afisa wa DCI na mwenzake John Kamau almaarufu Faruk, ambaye pia amejihami ndiyo washukiwa wakuu.

Konstebo David Mayaka aliuawa mnamo Agosti 10, kwa kupigwa risasi na majambazi watatu waliokuwa wamejihami katika eneo la Kayole, Kaunti ya Nairobi, alipokuwa akibadilisha tairi la gari lake akiwa na mkewe.