Al-Shabaab wawauwa watu 2,wachoma nyumba Lamu

Polisi walisema kuwa wawili hao waliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Nyongoro kwenye barabara kuu ya Witu-Lamu.

Muhtasari
  • Wavamizi hao walilenga lori moja kando ya barabara ya Lamu-Witu-Garsen eneo la Nyongoro, na kufyatua milio ya risasi kwenye gari hilo.

Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab walifanya shambulizi la kigaidi katika Kaunti ya Lamu usiku wa Jumatatu, Agosti 21 na kusababisha vifo vya watu wawili.

Wavamizi hao walilenga lori moja kando ya barabara ya Lamu-Witu-Garsen eneo la Nyongoro, na kufyatua milio ya risasi kwenye gari hilo.

Naibu kamishna wa kaunti ya Lamu Magharibi Gabriel Kioni alithibitisha kisa hicho akisema washambuliaji walitoroka.

"Gari hilo liliwekwa njiani na wanamgambo hao waliokuwa na silaha nzito kati ya 6.30 asubuhi na 7 asubuhi," alisema.

"Genge hilo lilitoroka mara baada ya tukio na juhudi za kukabiliana na tishio hilo zinaendelea."

Washambuliaji pia walikuwa wameteketeza takriban nyumba kumi katika Kijiji cha Salama, Kioni alisema.

Mashahidi na polisi walisema zaidi ya magaidi 30 waliokuwa na silaha nzito walivamia kijiji hicho kati ya saa 8.30 na 11 jioni mnamo Agosti 21.

Wasimamizi wa eneo hilo wamethibitisha kuwa magaidi hao pia waliiba mbuzi tisa, runinga, paneli za miale ya jua na taa kabla ya kukimbilia msitu wa karibu.

Kijiji cha Salama mnamo Juni mwaka huu kilivamiwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo walioua watu watano na kubomoa nyumba sita.

 

Polisi walisema kuwa wawili hao waliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Nyongoro kwenye barabara kuu ya Witu-Lamu.

Genge hilo lilikuwa limesimamisha magari kwenye eneo hilo na kuanza kuwashambulia waliokuwa ndani. Polisi walifika baadaye na kuwatawanya washambuliaji.