Mshukiwa wa mauaji ya afisa wa DCI Kayole apigwa risasi

Bastola ambayo iliripotiwa kutumika katika kumuua DCI Mayaka katika shambulizi huko Mihango mnamo Agosti 8 ilipatikana kutoka kwa mshukiwa.

Muhtasari

• Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia kisa hiki wanasema waliwaweka wawili hao kwenye eneo la uhalifu na kupata pikipiki iliyotumiwa kutorokea baada ya shambulizi lao.

crime scene
crime scene

Mshukiwa anayehusishwa na mauaji ya afisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai alipigwa risasi Jumanne asubuhi katika ufyatulianaji risasi uliotokea mtaani Kayole, Nairobi. 

Polisi walisema John Kamau almaarufu Faruk, aliuawa kwa risasi za polisi alipokuwa akipambana na kundi la wapelelezi waliokuwa wamemzuia katika maficho yake eneo la Soweto. Faruk alimpiga risasi na kumjeruhi mmoja wa maafisa waliokuwa wamekuja kumkamata na kusababisha wenzake wengine kufyatua risasi na kumuua.

Bastola ambayo iliripotiwa kutumika katika kumpiga risasi mpelelezi David Mayaka katika shambulizi huko Mihango mnamo Agosti 8 ilipatikana kutoka kwa mshukiwa. Polisi walisema bastola ya Ceska ilikuwa na risasi 12 ilipopatikana kutoka kwa Faruk. Mkuu wa polisi wa Nairobi, Adamson Bungei alisema afisa huyo aliyejeruhiwa alikimbizwa hospitalini akiwa katika hali thabiti. 

Katika oparesheni hiyo iliyoendeshwa na maafisa wa kitengo maalum kutoka makao makuu ya DCI mjini Nairobi, walimfuata Faruk nyumbani kwake Jumanne saa nne asubuhi. Waliizingira nyumba hiyo na kumwamuru ajisalimishe. Kulingana na Bungei, badala yake alianza kufyatua risasi na kumjeruhi afisa mmoja. 

“Hii iliwalazimu maafisa wengine kumjeruhi vibaya mshukiwa. Tulitaka akabiliane na idara za haki,” Bungei alisema. 

Polisi walikuwa wakimfuatilia Faruk kwa muda wa wiki kadhaa zilizopita baada ya yeye na watu wengine wawili kumpiga risasi na kumuua Mayaka katika shambulizi la kuvizia alipokuwa akibadilisha gurudumu la gari lake mnamo Agosti 8. Tangu wakati huo, amekuwa akihama kutoka nyumba moja hadi nyingine ndani ya Kayole.

Mshukiwa mwenzake Alex Wanjiru, 23, alikamatwa akiwa amejificha katika nyumba ya nyanyake huko Kikuyu, Kiambu.Alikamatwa mnamo Agosti 15. Polisi walisema alitoroka mtaa wa Kayole punde baada ya kisa hicho na kutafuta hifadhi katika nyumba ya nyanyake huko Ruthingiti, kaunti ndogo ya Kikuyu kabla ya maafisa wa upelelezi kumpata. 

Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia kisa hiki wanasema waliwaweka wawili hao kwenye eneo la uhalifu na kupata pikipiki iliyotumiwa kutorokea baada ya shambulizi lao.  Kupatikana kwa pikipiki hiyo kumejiri baada ya maafisa hao kufanya uchunguzi wa kina wa kitaalamu ambao ulimweka mtuhumiwa na wenzake eneo la tukio, wakati halisi wa mauaji hayo. 

Uchanganuzi wa kina uliofanywa na wataalam wa maabara katika Maabara ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Kitaifa ya DCI tangu wakati huo umehusisha bunduki iliyofyatua risasi aina ya C2, na matukio matano ya wizi yaliyopita jijini, bosi wa DCI Mohamed Amin alisema. 

Kufikia sasa, wapelelezi pia wamemtambua mshukiwa mwingine mmoja aliyehusika na mauaji Henry Njihia ambaye alitajwa kuwa mhalifu sugu.