Mwili wa mwanamke aliyedaiwa kunajisiwa wapatikana ukining'inia darini

Maafisa wa polisi waliyotembelea eneo la tukio walisema mwili wa marehemu ulikuwa na alama za kamba shingoni na nguo zake zilikuwa zimechafuka.

Muhtasari

•Mwili huo ulihamishwa hadi hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kericho, ambapo uchunguzi ulifanyika ili kubaini madai ya ubakaji.

Mwili wa marehemu
Mwili wa marehemu
Image: Instagram//Azam

Polisi wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 27 ulipatikana ukining'inia kwenye paa la nyumba yao baada ya kushukiwa ubakwa katika kijiji cha Ainamoi, Kaunti ya Kericho.

Mwili huo ulipatikana katika nyumba ya dadake wa kambo ambayo iko karibu na yake, polisi walisema. Polisi walisema wanachunguza mauaji na ubakaji katika kisa hicho cha Agosti 20.

Maafisa wa polisi waliyotembelea eneo la tukio walisema mwili wa marehemu ulikuwa na alama za kamba shingoni na nguo zake zilikuwa zimechafuka.

Mwili huo ulihamishwa hadi hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kericho, ambapo uchunguzi ulifanyika ili kubaini madai ya ubakaji.

Sampuli zilichukuliwa kwa uchunguzi zaidi na mwili ulihamishwa unahifadhiwa kwenye makafani.

Takwimu za polisi zinaonyesha kesi za ubakaji zinaongezeka vijijini huku kukiwa na kampeni za kukabiliana na tishio hilo.

Kwingineko katika soko la Nyabara Ibera ndani ya eneo dogo la Nyabisimba, Nyamira, mwili wa Steve Mokua Mongare, 30, ulipatikana kwenye barabara karibu na nyumba yake ya kupanga.

Polisi walisema mwili huo ulikuwa na majeraha kichwani. Mwanamke ambaye alikuwa akiishi pamoja na marehemu alikamatwa kwa mahojiano, polisi walisema.

Na katika kijiji cha Mukinye, Gatundu, Kaunti ya Kiambu, mwanamke mwenye umri wa miaka 49 ambaye alikuwa na kifafa alipatikana akiwa amefariki kwenye kitanda chake.

Polisi wanasema waliarifiwa kuwa Fidels Njahira Ndotono alipatikana akiwa amekufa kwenye kitanda chake akiwa amelala kifudifudi.

Mwili wake haukuwa na majeraha yoyote wakati polisi walipofika eneo la tukio kuuchukua mwili huo.