Mshtuko baada ya gunia 12 za bangi kupatikana zikisafirishwa kwenye gari la kubebea maiti, Busia

Gari jeupe aina ya Nissan Van lililobandikwa jina la Rafiki Funeral Services-Othaya ambalo lilikuwa limebeba shehena hiyo.

Muhtasari

•Gari hilo lilikuwa limezibwa kwa rangi nyingi na redio yake ilikuwa ikicheza nyimbo za huzuni zinazohusishwa na kumsindikiza marehemu.

•Kilo 58 nyingine za bangi zilizokuwa zikisafirishwa kwa pikipiki zilipatikana na polisi wa kituo cha Korondile, kaunti ya Wajir Jumapili jioni.

Image: TWITTER// DCI

Polisi katika Kaunti ya Busia  walibaki wamepigwa na butwaa Jumapili usiku baada ya kunasa shehena ya magunia 12 ya bangi iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea mjini Kisumu kwa gari la kubebea maiti.

Gari jeupe aina ya Nissan van lililobandikwa jina la Rafiki Funeral Services-Othaya ambalo lilikuwa limebeba shehena hiyo lilionekana na kuamriwa kusimama na maafisa waliokuwa wakisimamia kizuizi cha barabarani katika eneo la Suo mwendo wa saa moja jioni wakati likijaribu kuelekea katika jiji hilo la kando ya ziwa.

Kulingana na ripoti ya DCI, bangi iliyokuwa ikisafirishwa ilikuwa imepangwa vizuri ndani ya gari hilo lililokuwa limezibwa kwa rangi nyingi na ambalo redio yake ilikuwa ikicheza nyimbo za huzuni zinazohusishwa na kumsindikiza marehemu.

“Huku dereva wa gari hilo akishusha dirisha lake kwa kusitasita na kusema maneno machache baada ya kujibu salamu za afisa huyo, polisi huyo aligundua harufu fulani kutoka ndani ya gari ambayo haikuhusiana na mwili wa binadamu.

Hofu yake ilithibitishwa muda mfupi baadaye ambapo baada ya kufanya upekuzi ndani ya gari pamoja na wenzake, waligundua gunia 12 za bangi zikiwa zimepangwa kwenye viti na sakafu ya gari hilo,” ripoti ya DCI ilisoma.

Dereva, Bw Hussein Otita kisha alikamatwa na gari lake kuzuiliwa katika kituo cha polisi.

Kilo 58 nyingine za bangi zilizokuwa zikisafirishwa kwa pikipiki zilipatikana na polisi wa kituo cha Korondile, kaunti ya Wajir Jumapili jioni.

Washukiwa wawili, Osman Boru na Halkno Guchu walikamatwa na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Korondile wakisubiri kufikishwa mahakamani.

"Wapelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Madawa ya Kulevya, wamechukua uchunguzi wa kesi hizo mbili," DCI walisema.

Mapema mwezi huu, washukiwa wanne walitiwa mbaroni baada ya shehena kubwa ya bangi na shilingi milioni 13.4 pesa taslimu kupatikana katika mitaa ya mabanda ya Kariua, mtaa wa Ngara, jijini Nairobi.

Bi Teresia Wanjiru na vijana watatu wadogo wenye umri wa kati ya miaka 16 na 17 waliwekwa rumande kwa mahojiano zaidi kufuatia operesheni hiyo na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.