Waziri wa usalama Kithure Kindiki atoa onyo kwa magaidi na vikundi vya waalifu

Akizungumza huko Tana River, Kindiki alisema kuwa serikali haitalegea katika mipango yake ya kupambana na ugaidi.

Muhtasari

•Waziri wa usalama na Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amewapa magaidi na magenge ya wahalifu chaguzi tatu huku serikali ikithibitisha mapambano yake dhidi ya ugaidi.

•Alitangaza kuwa serikali itatuma vikosi maalum na vitengo vya wasomi Kaskazini mwa Kenya na maeneo ya Pwani ya Juu, zikiwemo Kaunti za Tana River na Lamu

Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki
Image: TWITTER

Waziri wa usalama na Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amewapa magaidi na magenge ya wahalifu chaguzi tatu huku serikali ikithibitisha mapambano yake dhidi ya ugaidi.

Akizungumza huko Tana River siku ya Jumatano, Kindiki alisema kuwa serikali haitalegea katika mipango yake ya kupambana na ugaidi.

"Kama vile rais alisema mambo ni matatu, ata mimi naambia magaidi mambo ni matatu. Wawachane na ugaidi, wahame Kenya warudi kwao ama tutawasafirisha safari ya njia moja,na si safari ya kwenda na gari , ni ya kwenda hadi wafikie jehanamu,"  alisema.

Waziri huyo alikuwa akizungumza alipokuwa akihutubia baraza la usalama Wayu, Kata Ndogo ya Galledertu, Kaunti ya Tana River.

Akiendelea zaidi, Kindiki aliweka mipango ya jinsi serikali itakavyokabiliana na ugaidi na itikadi kali kali.

Alitangaza kuwa serikali itatuma vikosi maalum na vitengo vya wasomi Kaskazini mwa Kenya na maeneo ya Pwani ya Juu, zikiwemo Kaunti za Tana River na Lamu,ambao watakabiliana na vikundi katili na kuwazuia wahalifu wenye silaha wanaowatishia raia wasio na hatia.

"Maafisa hawa wamefunzwa kukabiliana na wanamgambo wa aina hiyo. Hatuwezi kuruhusu wahalifu wa aina hiyo kutoka mataifa mengine na kuvuruga amani yetu, wamepewa mafunzo maalum kuhusu jinsi ya kukabiliana na wahalifu wakatili wakiwemo magaidi na majambazi,”

Mtu mmoja aliuawa na nyumba kadhaa kuchomwa moto katika shambulio la wanamgambo wa al Shabaab eneo la Widhu, kaunti ya Lamu.

Hili ni tukio la hivi punde zaidi kutokea katika eneo hilo huku kukiwa na ongezeko la operesheni za kukabiliana na tishio hilo linalohusiana na ugaidi.

Walioshuhudia walisema genge hilo lilichoma nyumba katika uvamizi huo kabla ya kutoroka. Hakuna aliyekamatwa.

Tukio hili lilifanyika Jumanne usiku kabla ya ziara ya  waziri Kindiki katika kaunti jirani ya Tana River siku ya Jumatano.

Tayari operesheni kubwa inaendelea katika eneo hilo ili kukabiliana na mashambulizi yanayohusiana na al-Shabaab, ambayo hutokea kwa sababu miongoni mwa mengine, ukaribu wa mpaka mkuu wa Kenya na Somalia.

Kando na hayo, Waziri Kindiki alisema vitengo hivyo maalum vimeagizwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kulinda Wakenya na ardhi yao.

Kindiki alisisitiza kuwa serikali imetangaza vita dhidi ya ugaidi na haitarudi nyuma.

“Tunawapigia saluti na kuwapa heshima maafisa wetu wa usalama wa mashirika mbalimbali ambao wameanguka katika majukumu yao, wakilinda taifa letu na watu wake dhidi ya wahalifu,” 

Kindiki aliweka wazi kuwa kiongozi yeyote anayechochea vurugu na uharibifu wa mali atakamatwa na kufunguliwa mashtaka, bila kujali nyadhifa zao za kisiasa.