Baraza la Usalama la UN laidhinisha azimio la Kenya kupeleka polisi Haiti

Kenya imeahidi angalau maafisa 1,000 wa polisi, na mataifa mengine kadhaa yanatarajiwa kutoa rasilimali nyingine.

Muhtasari

• Ripoti zinaonyesha kuwa magenge yanayofungamana na vyama vya siasa yameimarisha nguvu zao nchini humo tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mwaka wa 2021.

Bunduki
Bunduki
Image: Andrew Kasuku

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu, Oktoba 2, liliidhinisha mkakati wa mwaka mzima wa usalama wa kimataifa nchini Haiti, kuongozwa na Kenya, kukabiliana na machafuko ya magenge ambayo yamesababisha maafa ya watu wengi katika taifa hilo la Karibea.

Baraza hilo lenye wanachama 15 lilipiga kura kuidhinisha oparesheni ambayo ingelinda miundombinu muhimu kama vile viwanja vya ndege, bandari, shule, hospitali na maeneo muhimu ya barabara.

Pia watafanya "operesheni zinazolenga" pamoja na Polisi wa Kitaifa wa Haiti.

Kenya imeahidi angalau maafisa 1,000 wa polisi, na mataifa mengine kadhaa yanatarajiwa kutoa rasilimali nyingine.

Takriban watu 3,000 waliuawa nchini Haiti kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Juni, huku magenge yakiteka maeneo makubwa ya nchi hiyo, hususan Port-au-Prince, mji mkuu, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Vitongoji vingi vimesalia mahame huku watu wakikimbia mauaji, utekaji nyara na unyang'anyi.

Ripoti zinaonyesha kuwa magenge yanayofungamana na vyama vya siasa yameimarisha nguvu zao nchini humo tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mwaka wa 2021.

Hakuna uchaguzi wa manispaa, ubunge au wa kisiasa ambao umefanyika kwa miaka mingi, na hivyo kusababisha utupu wa mamlaka.afisa walisema lengo moja la ujumbe unaoongozwa na Kenya ni kuweka mazingira salama ya ya uchaguzi.

Kenya sasa itapeleka kikosi chake Haiti ifikapo Januari 2024.

Baraza lilipiga kura 13 kuunga mkono azimio hilo, huku Urusi na Uchina zikijisusia.

Waziri wa mambo ya nje wa Haiti, Jean Victor Généus, aliliita azimio hilo "mwanga wa matumaini" kwa watu ambao wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu sana.

"Hii ni zaidi ya kura rahisi," alisema.

"Hii, kwa kweli, ni ishara ya mshikamano na idadi ya watu walio katika dhiki."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken alipongeza kura hiyo.

"Tunapongeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha ujumbe wa Msaada wa Usalama wa Kimataifa nchini Haiti - hatua muhimu katika kutoa msaada wa kimataifa ulioombwa na Haiti kurejesha usalama. “Tunashukuru Kenya na Ecuador kwa ushirikiano wao mkubwa katika juhudi hizi,” alisema baada ya kura.

Kususia kwa Urusi na Uchina hakukuathiri matokeo ya kura.