Kenya iko tayari 'kuijenga upya' Haiti baada ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono

"Agizo hili sio tu kuhusu amani na usalama, lakini pia kuhusu ujenzi wa Haiti," Waziri Alfred Mutua alisema.

Muhtasari

•Waziri Mutua alitoa wito kwa washirika wa kimataifa kusaidia Kenya kuweka pamoja misheni yenye ufanisi ya usaidizi wa kimataifa.

Image: BBC

Kenya imesema kikosi cha usalama cha kimataifa kitatumwa Haiti "ndani ya muda mfupi" baada ya Umoja wa Mataifa kupiga kura kuunga mkono pendekezo la taifa hilo la Afrika Mashariki kuongoza ujumbe huo.

"Agizo hili sio tu kuhusu amani na usalama, lakini pia kuhusu ujenzi wa Haiti," Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Kenya Alfred Mutua aliandika ujumbe wake katika mtandao wa X (zamani ulijulikana kama Twitter).

Alitoa wito kwa washirika wa kimataifa kusaidia Kenya kuweka pamoja misheni yenye ufanisi ya usaidizi wa kimataifa "ambayo ndani ya muda mfupi, itakuwa nchini Haiti kubadilisha maisha".

Baadaye Jumatatu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kwa wingi kutumwa kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya kusaidia kupambana na ghasia za magenge nchini Haiti.

Azimio hilo liliidhinishwa kwa kura 13 za ndio na mbili za China na Urusi kutoshiriki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Haiti Jean Victor Geneus alipongeza kura hiyo ya Jumatatu, na kuitaja kama "kielelezo cha mshikamano na watu walio katika dhiki".

Bado haijabainika ni kiasi gani kikosi hicho kitakuwa kikubwa lakini Kenya imependekeza kutuma maafisa 1,000 wa polisi katika taifa hilo la Caribbean. Bahamas, Jamaica na Antigua and Barbuda wamesema watashiriki katika misheni hiyo.

Bw Mutua aliambia BBC kwamba alitarajia kikosi hicho kiwepo mwanzoni mwa mwaka ujao, "kama si kabla ya hapo".