Ruto aagiza kukamatwa kwa waliohusika na mapigano Sondu

Pia alibainisha kuwa maafisa wengine wote wa usalama watakaopatikana kuhusika katika mapigano hayo

Muhtasari
  • “Kuna watu wanaturudisha nyuma na tutawashughulikia sawa na tulivyowashughulikia majambazi wa North Rift na Al Shabaab,” alisema.
Rais Ruto kuongeza idadi ya watoza ushuru kwenye masoko, mitaa.
Rais Ruto kuongeza idadi ya watoza ushuru kwenye masoko, mitaa.
Image: Facebook

Rais William Ruto ameamuru kukamatwa kwa wale wote waliohusika na mapigano katika mpaka wa Kericho-Kisumu huko Sondu ambayo yamesababisha vifo vya watu saba.

Akizungumza huko Nyando, Kaunti ya Kisumu katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku 4 huko Nyanza, Ruto  alisema Kenya haina wakati wa watu walio na chuki za kikabila na kuagiza Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kuwachukulia hatua kali wahusika.

“Kuna watu wanaturudisha nyuma na tutawashughulikia sawa na tulivyowashughulikia majambazi wa North Rift na Al Shabaab,” alisema.

"Niwahakikishie kwamba kila mtu ambaye alisababisha mwananchi akapoteza maisha yake lazima akamatwe na apelekwe jela."

Waziri Kindiki mnamo Alhamisi aliwahamisha wakuu wa usalama kutoka pande zote za mpaka huku serikali ikichukua hatua kurejesha utulivu na kurudisha hali katika eneo hilo kuwa sawa.

Pia alibainisha kuwa maafisa wengine wote wa usalama watakaopatikana kuhusika katika mapigano hayo pia watahamishwa, na wahusika wa uhalifu huo kukamatwa.

Kindiki aliongeza kuwa timu ya mashirika ya ulinzi na usalama imetumwa Sondu.

“Jioni ya leo, serikali imetuma kikosi cha wana usalama maalumu ili kudhibiti ongezeko la uhalifu katika Mji wa Sondu na viunga vyake. Maisha ya watu yamepotea, mali kuharibiwa, na utaratibu wa raia kudhoofishwa sana katika siku mbili zilizopita,” alisema Alhamisi jioni.