Ruto: Tutashuhudia mvua kubwa, sio El Nino kama ilivyokadiriwa

Hii, Ruto alisema, ni nzuri kwa sekta ya kilimo nchini.

Muhtasari

•Ruto amesema nchi haitashuhudia mvua ya El Nino kama ilivyotabiriwa awali na Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya.

•Idara ya hali ya hewa ilikuwa imetahadharisha kuwa El Nino itaikumba nchi kutoka katikati ya Oktoba hadi Desemba.

akiwahutubia waumini katika eneo la Revival Sanctuary of Glory, Riruta Satellite, Dagoretti Kusini, Oktoba 22, 2023.
Rais William Ruto akiwahutubia waumini katika eneo la Revival Sanctuary of Glory, Riruta Satellite, Dagoretti Kusini, Oktoba 22, 2023.
Image: PCS

Rais William Ruto amesema nchi haitashuhudia mvua ya El Nino kama ilivyotabiriwa awali na Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya.

Rais badala yake alisema idara hiyo imepunguza makadirio yake hadi mvua kubwa lakini sio ya kusabisha uharibifu.

Hii, Ruto alisema, ni nzuri kwa sekta ya kilimo nchini.

Rais alizungumza wakati wa ibada ya kanisa katika eneo la Dagoretti Kusini siku ya Jumapili

"Hata juzi mliskia tukawa na habari pengine kutakuwa na El Nino ambaye itaharibu kule, itaharibu mali ingine lakini Mungu ni nani. Mmesikia wale watu wamesema tena ile El Nino haitakueko,” rais alisema.

"Wamesema kutakuwa tu na mvua kubwa lakini haitafika pale ya kuharibu. Si tunamshukuru mungu. Na hii mvua mingi ambayo tutapata tumejipanga, tumepang wakulima watuzalishie chakula,” Ruto alisema.

Idara ya hali ya hewa ilikuwa imetahadharisha kuwa El Nino itaikumba nchi kutoka katikati ya Oktoba hadi Desemba.

Hata hivyo, walifafanua kuwa mvua hiyo itakuwa kubwa.

Rais Ruto aidha alisema maombi ya mvua aliyofanyika katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo mnamo Februari pia yamezaa matunda.

"Nchi imekuwa na mvua za muda mrefu ambazo zimeruhusu wakulima kuzalisha zaidi kwa ajili ya nchi," alisema

"Wapo waliotulaumu wakati tunaomba mvua inyeshe. Sasa tuna mvua nyingi zaidi ya miaka minne, hiyo ni kazi ya Mungu."

Ruto pia aliahidi kuhakikisha serikali yake inaweka rasilimali na juhudi zaidi katika kilimo na uzalishaji wa chakula, ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini umehakikishwa.