Watahiniwa wawili wa KCSE wafariki baada ya kunywa Ethanol Tharaka-Nithi

Wanafunzi wengine 11, wakiwemo wasichana wanne na wavulana saba, wanapokea matibabu.

Muhtasari

•Wanafunzi wawili wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Karigini Mixed Day wamefariki dunia baada ya kunywa Ethanol.

•Wawili waliofariki walikuwa wamekunywa kiasi kikubwa cha ethanol lakini pengine wangeokolewa ikiwa wangetafuta matibabu mara moja.

Rip
Rip
Image: HISANI

Wanafunzi wawili wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Karigini Mixed Day wamefariki dunia baada ya kunywa Ethanol kutoka katika maabara ya shule hiyo.

Watahiniwa hao wawili wanatoka Tharaka Nithi.

Timu ya wapelelezi kutoka Nairobi wameungana na wale waliokuwa mashinani kuchunguza suala hilo, polisi walisema.

Kamanda wa polisi kaunti ya Tharaka Nithi Zacchaeus Ngeno alisema wanafunzi wengine 11, wakiwemo wasichana wanne na wavulana saba, wanapokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Chuka, ambapo walipelekwa Jumamosi alasiri.

“Tumeambiwa wanafunzi walikunywa kemikali hiyo Alhamisi jioni lakini ni mmoja tu aliyeonyesha dalili za kizunguzungu mara moja. Tumegundua kuwa ndiyo sababu ya vifo hivyo,” alisema.

Bosi huyo wa polisi alisema wakati timu ya maafisa wa usalama, elimu na afya ilipotembelea shule hiyo Jumamosi asubuhi waliweza kubaini kupitia wanafunzi wengine waliotumia dawa hiyo kuwa ni ethanol.

Hata hivyo, alisema uchunguzi bado unaendelea kuhusu suala hilo na atabainisha zaidi.

Wachunguzi walichagua sampuli za kemikali kwa uchambuzi zaidi.

"Uchunguzi wa maiti na vipimo kwa walio hospitalini utatuambia zaidi. Ngoja tusubiri,” alisema.

Alisema wawili waliofariki walikuwa wamekunywa kiasi kikubwa cha ethanol lakini pengine wangeokolewa ikiwa wangetafuta matibabu mara moja.

"Waliofariki walikimbizwa hospitalini Jumamosi asubuhi baada ya afya zao kuzorota," alisema.

Maafisa wa hospitali hiyo walisema ingawa waliolazwa wanaendelea vizuri, wataendelea kuwa hospitalini kwa muda huku wakiendelea kuangaliwa kwa sababu hata wawili waliofariki walikuwa katika hali nzuri hadi Ijumaa jioni walipofariki.

Maafisa zaidi walitarajiwa kuzuru taasisi hiyo Jumapili kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea.

Walisema watarekodi taarifa kutoka kwa wanafunzi na walimu.

Timu hiyo pia itazungumza na wanafunzi wengine na kuwahakikishia usalama wao, maafisa walisema huku kukiwa na wasiwasi kutoka kwa wazazi na walezi.

Haya yanajiri huku shule hiyo na nyingine zikifanya mazoezi ya mitihani yao ya kitaifa.

Viongozi wengine wamehimiza umakini zaidi shuleni ili kuepusha mikasa hiyo.

Shule huhifadhi kemikali ikiwa ni pamoja na ethanol na kutumika katika maabara.