Shilingi ya Kenya yasajili thamani ya chini mno katika hostoria dhidi ya dola

Benki Kuu ya Kenya (CBK) iliweka thamani ya shilingi kwa dola kwa kiwango cha 149.94 siku ya Jumatatu.

Muhtasari

• Kulingana na benki kuu, sarafu ya Kenya imeshuka thamani baada ya muda dhidi ya sarafu kuu za kimataifa na kikanda, ikibadilishana na pauni kwa kiwango cha chini cha shilingi 182.08.

Image: MAKTABA

Shilingi ya Kenya ilishuka hadi kiwango cha chini mno kuwahi kusajiliwa katika historia ya Kenya hadi 150 dhidi ya dola ya Marekani siku ya Jumatatu. 

Hali hii imeongeza shinikizo na kusababisha kupungua kwa hifadhi ya fedha za kigeni nchini Kenya na kupandisha gharama ya uagizaji bidhaa huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei. 

Benki Kuu ya Kenya (CBK) iliweka thamani ya shilingi kwa dola kwa kiwango cha 149.94 siku ya Jumatatu, kuashiria kudorora kwa asilimia 24 kwa thamani ya shilingi ya Kenya katika kipindi cha mwaka sasa. 

Akiba ya fedha za kigeni mnamo Oktoba 19 ilifikia kiwango cha chini zaidi cha dola za Kimarekani bilioni 6.83, ambazo ziligharimu uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.67, kushuka kutoka dola bilioni 7.29 mwaka mmoja uliopita. 

Benki kuu, katika ripoti yake ya hivi punde ya uthabiti wa sekta ya fedha iliyotolewa Oktoba 15, ililaumu kudorora kwa sarafu ya Kenya kutokana na "kubanwa kwa sera za kifedha kwa kasi hali iliyosukuma viwango vya riba vya kimataifa kupanda juu." 

Kulingana na benki kuu, sarafu ya Kenya imeshuka thamani baada ya muda dhidi ya sarafu kuu za kimataifa na kikanda, ikibadilishana na pauni kwa kiwango cha chini cha shilingi 182.08 na euro kwa shilingi 158.54 Jumatatu. 

Mfumuko wa bei nchini ulipanda hadi asilimia 6.8 mwezi Septemba, likiwa ni ongezeko la kwanza tangu Mei, kutoka asilimia 6.7 mwezi Agosti.