SGR yapandisha nauli, Nairobi-Mombasa ni Sh1,500 kuanzia Januari

Shirika la Reli la Kenya limeongeza nauli kwa njia zote kwa asilimia 50

Muhtasari

•Kwa wale wanaotaka kusafiri na daraja la kwanza, watalazimika kulipa Sh4,500, kutoka Sh3,000

 Kampuni ya Kenya Railways imeongeza nauli katika  maeneo yote inayohudumu kwa asilimia 50.

Katika hakiki ya hivi punde, abiria wa Mombasa sasa watalipa Sh1,500 kuanzia Januari 1, 2024, kutoka Sh1,000 ya sasa.

Tikiti zilizonunuliwa kabla ya wakati huo, hata hivyo, hazitaathirika.

"Wateja wanaofanya ununuzi wa mapema wa Huduma ya Abiria ya Madaraka Express watatambua nauli zilizorekebishwa kuanzia Novemba 1, 2023," wasimamizi walisema.

Kwa wale wanaotaka kusafiri na daraja la kwanza, watalazimika kulipa Sh4,500, kutoka Sh3,000.

Nauli kutoka Kibwezi hadi Mombasa itagharimu Sh890 huku Voi hadi Mombasa ikigharimu Sh440.

Bei hizo ziliorodheshwa upya kwa Huduma ya abiria wa Madaraka Express, Huduma ya Reli ya Nairobi Commuter, Treni ya Safari ya Kisumu na Treni ya Safari ya Nanyuki.