KNEC yavunja kimya baada ya Wakenya kushindwa kuangalia matokeo ya KCPE 2023 kupitia sms

KNEC imeomba radhi kwa Wakenya kupitia ujumbe wa SMS kuhusu kucheleweshwa kwa matokeo.

Muhtasari

•Ingawa wizara haikutoa muda kamili ambao tatizo hilo litatatuliwa, ilisema mafundi wake wanashughulikia suala hilo.

•KNEC ilisema kuwa watatoa sasisho mara tu nambari ya kuangalia matokeo (40054) itakapoanza kufanya kazi.

 

akimkabidhi matokeo ya KCPE kwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu wakati wa kuchapishwa kwa matokeo ya mtihani wa KCPE wa 2023 katika jumba la New Mitihani House mnamo Novemba 23, 2023.
Mwenyekiti wa KNEC Prof Julius Omondi Nyabundi akimkabidhi matokeo ya KCPE kwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu wakati wa kuchapishwa kwa matokeo ya mtihani wa KCPE wa 2023 katika jumba la New Mitihani House mnamo Novemba 23, 2023.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Wizara ya Elimu ya Kenya imetangaza kuwa inajitahidi kuhakikisha nambari ya SMS ya kuangalia matokeo ya KCPE 2023 (40054)  inafanya kazi.

Hii ni baada ya watahiniwa, wazazi na washika dau wengine kulalamika kwamba haifanyi kazi walipojaribu kupata matokeo yao siku ya Alhamisi.

Maelfu wametumia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine kueleza kusikikishwa kwao wakitaja kwamba hawajapokea matokeo hata baada ya majaribio kadhaa ya kutuma nambari ya mtihani kwa nambari 40054 iliyotolewa na wizara ya elimu.

Wakenya waliokuwa wamejaribu kuangalia matokeo kupitia sms walikuwa wakipata arifa, “Mpendwa Mteja, matokeo ya KCPE 2023 hayapatikani. Tafadhali jaribu tena baadaye baada ya tangazo. Nambari ya usaidizi ya KNEC 08007224900."

Ingawa wizara haikutoa muda kamili ambao tatizo hilo litatatuliwa, ilisema mafundi wake wanashughulikia suala hilo.

Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC) pia limeomba radhi kwa Wakenya kupitia ujumbe wa SMS kuhusu kucheleweshwa kwa matokeo.

Katika ujumbe huo uliotumwa kwa watu wengi, KNEC ilisema kuwa watatoa sasisho mara tu nambari ya kuangalia matokeo (40054) itakapoanza kufanya kazi.

“Salamu, tunaomba radhi kwa kuchelewa kupata matokeo ya KCPE 2023. Tutakujulisha pindi zitakapopatikana kwa 40054,” ulisomeka ujumbe huo uliotumwa na KNEC kwa Wakenya kupitia njia ya sms.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alitangaza rasmi matokeo ya mitihani ya KCPE 2023 mnamo Alhamisi asubuhi.

Waziri huyo alitangaza matokeo katika Mtihani House akiwa na wadau wa elimu akiwemo waziri wa kudumu Belio Kipsang, na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Huduma kwa Walimu Nancy Macharia, miongoni mwa wengine.

Katika matokeo hayo, jumla ya watahiniwa 8,525 walipata alama 400 na zaidi, ambayo waziri alisema ni sawa na asilimia 0.60%.

Katika nafasi ya alama kati ya 300 na 399, kulikuwa na watahiniwa 352,782, ikiwa ni asilimia 24.29.

Aidha, Machogu alisema jumla ya watahiniwa 658,278  ambao ni sawa na  48.49% walipata alama kati ya 200 na 299.

Pamoja na hayo, jumla ya watahiniwa 383,025 walipata alama kati ya 100 hadi 199, ambayo ni sawa na 27.05% ya watahiniwa.

Watahiniwa 2,060 walipata alama kati ya 001 na 099.