Watahiniwa 133 wa KCPE walipewa alama zisizo sahihi katika baadhi ya masomo - Knec

"Knec imekagua malalamishi yote na kugundua kuwa kulikuwa na watahiniwa 133 walioathirika," Njengere alisema.

Muhtasari

•KNEC imekiri kwamba kuna watahiniwa 133 ambao walipewa alama zisizo sahihi katika mtihani wa KCPE 2023.

•Njengere alishauri wanafunzi watembelee shule zao ili kupata matokeo yao kwa kuwa baadhi ya yale yanayotumwa kupitia SMS yana makosa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia, Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi Belio Kipsang, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, Mkurugenzi Mtendaji wa KNEC David Njengere na Mwenyekiti wa KNEC Julius Nyabundi wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCPE katika ofisi za KNEC kando ya Barabara ya Dennis Pritt Kilimani, Nairobi mnamo Desemba. 21, 2022
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia, Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi Belio Kipsang, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, Mkurugenzi Mtendaji wa KNEC David Njengere na Mwenyekiti wa KNEC Julius Nyabundi wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCPE katika ofisi za KNEC kando ya Barabara ya Dennis Pritt Kilimani, Nairobi mnamo Desemba. 21, 2022
Image: ANDREW KASUKU

Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya limekiri kwamba kuna watahiniwa 133 ambao walipewa alama zisizo sahihi katika mtihani wa KCPE 2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa Knec David Njengere mnamo Jumamosi alisema wamekuwa wakipokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya shule zilizoathiriwa kuhusu kutoridhika na matokeo yao kama yalivyopokelewa kupitia nambari ya SMS 40054.

Njengere alisema Knec pia ilipokea maswali kutoka kwa watahiniwa waliopata alama za chini katika baadhi ya masomo hasa ya Kiingereza na Kiswahili.

"Knec imekagua malalamishi yote na kugundua kuwa kulikuwa na watahiniwa 133 walioathirika."

Njengere alitoa hakikisho kuwa kesi zote 133 zimeshughulikiwa na matokeo ya watahiniwa walioathiriwa kurekebishwa ipasavyo.

Zaidi ya hayo, bosi huyo wa Knec alifichua kuwa matokeo ya baadhi ya watahiniwa yaliwekwa vibaya na alama za Kiswahili kuwekwa katika sehemu ya Lugha ya Ishara ya Kenya.

Aidha alisema kuna matukio ambapo alama za Sayansi na Social Studies na Elimu ya Dini yalikatwa kimakosa na kukosa alama za kuongeza (+) na kutoa (-) kama ilivyotarajiwa.

"Hitilafu hiyo iliathiri matokeo ya SMS pekee kutokana na masuala ya usanidi kwani matokeo katika tovuti ya KNEC ni sahihi," Njengere alisema.

Alisema Knec iliarifu mtoa huduma wa SMS na hitilafu katika jumbe hizo ilitatuliwa mara moja.

Njengere alishauri kwamba wanafunzi watembelee shule zao ili kupata matokeo yao ya muda kwa kuwa baadhi ya yale yanayotumwa kupitia SMS yana makosa.

"Watahiniwa wameshauriwa kutembelea shule zao na kukusanya hati rasmi za matokeo ya muda na kuuliza swali lolote kwa ajili ya kuhakiki matokeo yao, kama yapo, ndani ya muda wa siku 30 uliopangwa," Njengere alisema.

Wizara ya Elimu ilitoa matokeo ya mtihani wa KCPE wa 2023 wa 1,406,557 mnamo Jumatano, Novemba 23.

Mtahiniwa bora amepata alama 428.