Polisi wanachunguza kisa ambapo Padre mmoja alipatikana akiwa amefariki - Nairobi

Kulingana na polisi, mwili huo haukuwa na majeraha yoyote wakati huo ukihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Muhtasari

• Mlezi katika nyumba hiyo aliripoti kwa polisi kwamba mzee huyo mwenye umri wa miaka 88 alipatikana bila kuitikia baada ya kujaribu kumwamsha jumapili  bila mafanikio

• Polisiwaliripoti kuwa bado hawajajua chanzo cha kifo hicho na uchunguzi wa maiti utafichua zaidi.

Crime Scene
Image: HISANI

Polisi wanachunguza kisa ambapo kasisi mmoja mzee alipatikana akiwa amefariki katika nyumba yake huko Gigiri, Nairobi.

Mlezi katika nyumba hiyo aliripoti kwa polisi kwamba mzee huyo mwenye umri wa miaka 88 alipatikana bila kuitikia baada ya kujaribu kumwamsha jumapili  bila mafanikio.

Mlezi huyo aliripoti kuwa kasisi huyo amekuwa akipambana na matatizo ya shinikizo la damu.

Polisi walitembelea eneo la tukio na kusaidia kupeleka mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi wa maiti na taratibu nyinginezo.

Kulingana na polisi, mwili huo haukuwa na majeraha yoyote wakati huo ukihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Polisiwaliripoti kuwa bado hawajajua chanzo cha kifo hicho na uchunguzi wa maiti utafichua zaidi.

Kwingineko huko Msambweni, Kwale, polisi wanasaka genge lililomvamia na kumuua mlinzi aliyekuwa zamu katika tukio la wizi katika duka moja.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Kenya Loma Vitsangalaweni Junction, polisi walisema.

Mmiliki wa duka hilo alikwenda kulifungua Jumapili asubuhi na kushindwa kupata majibu kutoka kwa mlinzi wake kama kawaida.

Baadaye aligundua kuwa kituo hicho kilikuwa kimevunjwa na watu wasiojulikana.

Aligundua wezi hao waliiba shehena kumi  za  unga wa mahindi na kiasi cha pesa kisichojulikana.

Hapo ndipo alipogundua mlinzi wake aliyekuwa zamu hayupo na alipomchunguza aligundua kuwa alikuwa amelazwa  nyuma ya duka.

Polisi walisema mwili wa Gereza Katembo Bechuye, 40, ulikuwa na majeraha makubwa kichwani.

Mwili wake ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri kufanyiwa uchunguzi na wa maiti.

Polisi walitembelea eneo la tukio siku ya Jumapili kama sehemu ya uchunguzi wa mauaji uliosababishwa na wizi wa mabavu.

Hakuna aliyekamatwa kufikia sasa, polisi walisema  timu ya wapelelezi inafuatilia suala hilo