Habari za hivi sasa! Mahakama yafutilia mbali ushuru wa nyumba

Seneta wa Busia Okiya Omtatah na wengine sita walifika mahakamani wakitaka kusimamisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya 2023.

Muhtasari

• Jopo la majaji watatu liliafikia uamuzi kuwa sheria iliyotumika kutoza wakenya ushuru wa nyumba haikufuata taratibu za kisheria.

• Malalamishi mbalimbali yaliwasilishwa kupinga Sheria hiyo iliyoanza kutumika Julai 1 kabla ya Jaji Mugure Thande kutoa maagizo ya kusimamisha utekelezaji wake

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mahakama imefutilia mbali ushuru wa nyumba uliokuwa umeanza kutozwa na serikali.

Jopo la majaji watatu likiongozwa na jaji David Majanja liliafikia uamuzi kuwa sheria iliyotumika kutoza wakenya ushuru wa nyumba ilitekelezwa kwa njia isiyofaa.

Jopo la majaji David Majanja, Christine Meoli na Lawrence Mugambi lilisema kwamba serikali ilikosa kufuata kanuni za kisheria kabla ya KRA kuanza kuwatoza wakenya na waajiri asilimia 3 kila mwezi. 

Kulingana na mahakama wananchi hawakushirikishwa vya kutosha  kabla ya sheria hiyo kuwasilishwa katika bunge.

Baada ya majaji kutoa uamuzi wao mawakili wa upande wa walalamishi waliomba mahakama kuishurutisha serikali kuwarejeshea wakenya pesa ambazo tayari wamekatwa chini ya sheria hiyo. 

Mawakili wa upande wa serikali hata hivyo wameiomba mahakama kuipa serikali siku 45 zaidi iendelee kutekeleza sheria hiyo huku wakiwasilisha rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama.

Mswada wa Fedha wa 2023 ulipitishwa na bunge mnamo Juni 22, 2023, na baadaye kuidhinishwa na Rais William Ruto mnamo Juni 26.

Mahakama Kuu baadaye ilisitisha utekelezaji wa sheria hiyo mnamo Juni 30, baada ya maombi mengi kuwasilishwa.

Mnamo Julai 29, jopo la jaji Majanja liliondoa  agizo la mahakama kuu na kuruhusu serikali kuanza kutoza ada hizo. 

Seneta wa Busia Okiya Omtatah na wengine sita walifika mahakamani wakitaka kusimamisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya 2023.