Ushuru wa nyumba, Sifuna awaambia Wakenya kutosherehekea kusubiri rufaa

Jopo la majaji watatu lilitangaza ushuru wa nyumba ulioletwa na Rais William Ruto kuwa kinyume cha katiba.

Muhtasari

•  Sifuna alisema Wakenya wanapaswa kusubiri hadi pale suala hilo litakapoamuliwa na mahakama za juu.

• "Kuhusu ushuru wa nyumba, mnapaswa kusubiri hadi suala litakapofuata mkondo uongozi mzima wa Mahakamandiposa msherehekee, mimi ndiye ninawaambia," 

SENETA WA NAIROBI
Image: TWITTER// EDWIN SIFUNA

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amewashauri Wakenya kutosherehekea bado, kuhusu uamuzi wa mahakama ulioharamisha ushuru wa nyumba.

Kupitia ukurasa wake wa  X, Sifuna alisema Wakenya wanapaswa kusubiri hadi pale suala hilo litakapoamuliwa na mahakama ya  rufaa na hata mahakama ya upeo.

"Kuhusu ushuru wa nyumba, mnapaswa kusubiri hadi suala litakapofuta mkondo wote wa Mahakama ndiposa msherehekee, mimi ndiye nawaambia," alisema.

Uongozi wa mahakama unatoa nafasi kwa Serikali kwenda Mahakama ya Rufaa ili kupinga uamuzi huo na kisha Mahakama ya Juu Zaidi.

Jopo la majaji watatu lilitangaza ushuru wa nyumba ulioletwa na Rais William Ruto kuwa kinyume cha sheria.

Jopo hilo lililoongozwa na Jaji David Majanja,Christine Meloi na Jaji Lawrence Mugambi liliteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome

Majaji hao waliamua kwamba kuanzishwa kwa ushuru huo kulikuwa na ubaguzi kwa kuwa ilitoza ushuru kwa Wakenya wanaolipwa mishahara  pekee na kuwatenga wale wanaofanya kazi katika sekta zisizo rasmi.

 “Amri imetolewa ya kumzuia mlshtakiwa kutokusanya, au kutoza vinginevyo Sheria ya Nyumba Zinazouzwa kwa bei nafuu kwa misingi ya kifungu cha 84 cha Sheria ya Fedha na maombi yote husika” Jaji Majanja alisema.

Ushuru huo ulianza kutozwa baada ya  kupitishwa kwa Sheria ya Fedha, 2023.

Serikali iliteua Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) kama wakala wa kukusanya mapato, na ukusanyaji wake ulirejeshwa hadi Julai 1, 2023.

Waajiri wamekuwa wakituma mchango wao wa asilimia 1.5 pamoja na kiwango sawa kwa wafanyakazi wao kama tozo ya Nyumba.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah na mashirika mengine sita walikuwa wamefika kortini wakitaka kusimamisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha, 2023.