Huu umekuwa mwaka mgumu, Kalonzo asema akiadhimisha siku ya kuzaliwa ya 70

''Huu umekuwa mwaka mgumu sana kwa wengi wetu, lakini Mungu amejitokeza kila mara kwa ajili yetu,'' Kalonzo alisema.

Muhtasari

•Kalonzo alitimiza miaka 70 huku Wakenya wakiungana na wengine kote ulimwenguni kujiandaa kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

•Baadhi ya vinara wa chama cha Wiper walim’surprise Kalonzo kwa keki ya siku ya kuzaliwa katika makazi yake jijini Karen, Nairobi.

kabla ya kukata keki kusherehekea siku yake ya kuzaliwa 70
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Mbunge wa Kathiani Robert Mbui kabla ya kukata keki kusherehekea siku yake ya kuzaliwa 70
Image: HISANI

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka mnamo siku ya Jumapili alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 70 inayoambatana na mkesha wa Sikukuu ya Krismasi.

Makamu huyo wa zamani wa rais aliadhimisha miaka 70 huku Wakenya wakiungana na wengine kote ulimwenguni kujiandaa kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Kalonzo alihudhuria ibada ya kanisa la Nairobi Baptist Church siku ya Jumapili kabla ya washirika wake kumfanyia karamu ya kifana ya siku yake ya kuzaliwa.

''Huu umekuwa mwaka mgumu sana kwa wengi wetu, lakini Mungu amejitokeza kila mara kwa ajili yetu,'' Kalonzo alisema katika akaunti yake ya X.

''Hakika ujumbe kwamba kadiri tunavyotumia muda mwingi pamoja na Yesu, ndivyo antena yetu inavyopatana Naye, ulikuwa wa kusisimua sana.''

Baadaye baadhi ya vinara wa chama cha Wiper walim’surprise Kalonzo kwa keki ya siku ya sherehe katika makazi yake jijini Karen, Nairobi.

Mbunge wa Kathiani na naibu kiongozi wa wachache Robert Mbui alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Wiper waliojiunga na Kalonzo wakati wa sherehe ya kuzaliwa huko Karen.

Kalonzo alizaliwa Desemba 24, 1953, na aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa kumi wa Kenya kuanzia 2008 hadi 2013.

Kalonzo alihudumu katika serikali chini ya hayati Rais Daniel Arap Moi kama Katibu wa chama cha Kenya African National Union kati ya 1980 na 1988).

Pia aliwahi kuwa Waziri msaidizi wa Ujenzi (1986-1988), Naibu Spika wa Bunge (1988-1992), Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia 1993 hadi 1998 na Waziri wa Elimu (1998-2001).

Chini ya hayati Rais Mwai Kibaki, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje tena kutoka 2003 hadi 2004 na kisha Waziri wa Mazingira kutoka 2004 hadi 2005.

Alikuwa mgombea ambaye hakufanikiwa katika uchaguzi wa urais wa 2007, ambapo aliteuliwa kuwa makamu wa rais na Kibaki mnamo Januari 2008.