Mwanadada aliyerekodiwa akimtusi mhudumu wa hospitali ya Busia atiwa mbaroni

Bi Vanessa Ogema atashtakiwa kwa fujo anazodaiwa kusababisha hospitali ya Port Victoria siku kadhaa zilizopita.

Muhtasari

•Polisi walimkamata na kumzuilia mwanadada aliyerekodiwa kwenye videoakimtusi mhudumu wa hospitali mapema mwezi huu.

•Mshukiwa anadaiwa kutenda kosa la kuzua fujo kwa njia ambayo ingeweza kusababisha uvunjifu wa amani kinyume na sheria.

alikamatwa Januari 7, 2024.
Bi Vanessa Ogema alikamatwa Januari 7, 2024.
Image: TWITTER// DCI

Polisi katika Kaunti ya Busia mnamo siku ya Jumapili walimkamata na kumzuilia mwanadada aliyerekodiwa kwenye video iliyosambaa mtandaoni akimtusi mhudumu wa hospitali mapema mwezi huu.

Katika taarifa ya Jumapili jioni, Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) iliripoti kwamba Bi Vanessa Ogema atafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu, Januari 8, ambapo atashtakiwa kwa fujo anazodaiwa kusababisha hospitali ya Port Victoria siku kadhaa zilizopita.

“Vanessa Ogema mwenye umri wa miaka 23 ambaye alirekodiwa akimtusi mhudumu wa hospitali huku akitatiza utaratibu wa utoaji huduma katika Hospitali ya Port Victoria huko Busia amekamatwa. Mshukiwa atafikishwa mahakamani Jumatatu tarehe nane,” DCI ilisema kwenye taarifa.

Kulingana na bango la DCI, mshukiwa anadaiwa kutenda kosa la kuzua fujo kwa njia ambayo ingeweza kusababisha uvunjifu wa amani kinyume na sheria.

Wakenya katika wiki ya kwanza ya 2024 walionekana kukerwa na video ya kutatanisha ya binti huyo mwenye umri wa miaka 23 aliyedaiwa kumtishia mhudumu wa afya katika Hospitali ya Port Victoria, Kaunti ya Busia.

Video hiyo ilinasa mwanamume akijiandaa kumhudumia mgonjwa, na mwanadada huyo aliyedaiwa kutumia lugha isiyofaa kwa nesi wa kike.

Katika video hiyo, mwanamke huyo ambaye amekuja kutambulishwa kama Vanessa Ogema alinaswa akitupa vitu kutoka kwa dawati la muuguzi huku akidaiwa kurusha matusi.

Wakati mmoja, alijaribu hata kumkabili muuguzi, akirusha cheche za maneno na kuendelea kutatiza eneo la kazi la mhudumu wa afya kwa kurusha vitu.

Mwanamke huyo alinaswa kwenye kamera akitishia kumpigia mtu simu huku mwanamume huyo pia akipiga simu na mtu mwingine, akitaka wawepo kwenye kituo hicho.

“Harakisha ukuje hapa saa hii,” alisikika akisema kwenye simu.

Wakati huu, wawili hao walitazama chumba na kugundua kuwa walikuwa wakirekodiwa na kuondoka eneo la tukio.

Ripoti zinaonyesha kuwa watu hao wawili walikuwa wamemleta mtu kwenye kituo hicho na walitaka uangalizi wa haraka, hata mbele ya wagonjwa wengine ambao tayari walikuwa wakisubiri matibabu.

Walipofahamishwa kuwa hawawezi kuruka foleni, inasemekana walizua fujo na kutaja jina la afisa wa serikali.