Kunani? Safaricom yavunja ukimya kuhusu tatizo la M-pesa

Kampuni hiyo ilieleza kuwa matatizo ya kiufundi yanayoathiri huduma ya pesa kwa simu ya mkononi yalikuwa yameibuka.

Muhtasari

• Safaricom ilikiri kuwa huduma ya pesa kwa njia ya simu ilikuwa imekwama na kueleza kuwa tatizo hilo linatatuliwa.

Image: X/SAFARICOM

Kampuni kubwa zaidi ya kutoa huduma za simu za mkononi nchini Kenya, Safaricom PLC imevunja kimya kufuatia malalamiko ya Wakenya wengi kuhusu huduma za M-pesa.

Idadi kubwa ya watumiaji wa simu walikumbana na matatizo walipokuwa wakijaribu kutumia huduma za kutuma na kupokea pesa za M-pesa siku ya Jumanne asubuhi kwa kuwa miamala ilikuwa ikikosa kukamilika.

Wateja walipokea ujumbe wa arifa, “MPESA ina ucheleweshaji, na haiwezi kukubali ombi lako. Tafadhali subiri kwa dakika 10 kabla ya kujaribu tena,” kila walipojaribu kufanya miamala.

Watumiaji wengi wa MPESA walitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kuwasilisha malalamishi yao kwa kampuni ya Safaricom  kuhusu huduma ya kutuma na kupokea pesa na kutafuta majibu kwa tatizo hilo.

"MPESA iko chini @safaricom_care @SafaricomPLC," mtumiaji wa Twitter @saagyn aliandika.

Katika jibu lake, Safaricom ilikiri kuwa huduma ya pesa kwa njia ya simu ilikuwa imekwama na kueleza kuwa tatizo hilo lilikuwa likitatuliwa.

“Hujambo. Tunasikitika kuwa kuna hitilafu kwa ujumla inayoathiri huduma za M-PESA kwenye STK na APP. Hili linashughulikiwa kwa kipaumbele cha hali ya juu. Samahani kwa usumbufu uliojitokeza,” kampuni hiyo ilijibu.

Kampuni hiyo ilieleza kuwa matatizo ya kiufundi yanayoathiri huduma ya pesa kwa simu ya mkononi yalikuwa yameibuka.