Tanzia! 15 wafariki katika ajali mbaya kwenye barabara ya Nakuru-Eldoret

Watu wengine 38 walinusurika na majeraha katika ajali hiyo mbaya iliyohusisha basi na matatu.

Muhtasari

•Watu 15 walipoteza maisha yao usiku wa kuamkia Jumanne, Januari 9, kufuatia ajali mbaya iliyotokea kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Image: TWITTER// NPS

Watu 15 walipoteza maisha yao usiku wa kuamkia Jumanne, Januari 9, kufuatia ajali mbaya iliyotokea kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Watu wengine 38 walinusurika na majeraha katika ajali hiyo mbaya iliyohusisha basi la Classic Kings of Congo na matatu aina ya Toyota ya North Ways Shuttle.

Kulingana na Tume ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), kisa hicho ambacho kiliacha magari hayo mawili yakiwa yameharibika vibaya kilitokea mwendo wa saa tisa kasorobo asubuhi kuamkia siku ya Jumanne.

Manusura wa ajali hiyo walikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Molo.

"Huduma ya Kitaifa ya Polisi inawaomba madereva wote wa magari kuwa waangalifu sana katika barabara zetu ili kuzuia ajali za barabarani," NPS ilisema katika taarifa Jumanne asubuhi.

Waliambatanisha taarifa hiyo na picha za basi hilo la Classic Kings of Congo lililogonga vibaya na matatu ya viti 14.

Polisi walithibitisha kuwa watu wote waliokuwa kwenye matatu hiyo walipoteza maisha yao.

Abiria watatu wa basi walipata majeraha mabaya, huku wengine kumi wakipata majeraha madogo.

Polisi kutoka Mau Summit walijibu mara moja, na kusaidia kuwahamisha majeruhi hao hadi Hospitali ya Molo. Mkuu wa polisi wa Bonde la Ufa Tom Odero alisema kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea.

"Ilikuwa asubuhi nyingine ya kusikitisha ambapo tumepoteza watu 15. Wengine wamejeruhiwa na wako hospitalini,” alisema.

Odero alitoa wito kwa madereva wote kuchukua tahadhari wawapo barabarani ili kuzuia ajali za barabarani.