Watu wengine 22 wajeruhiwa katika ajali kwenye barabara ya Nairobi–Nakuru

Wengi wa abiria walikuwa wanafunzi waliokuwa wakirejea shuleni.

Muhtasari

•St John ilisema ajali hiyo ya siku ya Jumatano ilitokea baada ya matatu ambayo wanafunzi hao walikuwamo kugongana na lori uso kwa uso.

•Kisa hicho kinajiri siku moja baada ya watu 15 kufariki katika ajali iliyotokea katika Barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

lililohusika katika ajali karibu na Keroche kwenye Barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.
Gari lililohusika katika ajali karibu na Keroche kwenye Barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.
Image: ST JOHN'S AMBULANCE

Takriban watu 22 wamepata majeraha baada ya ajali kutokea katika eneo la Karai, karibu na Keroche kwenye Barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.

Kulingana na St John Ambulance, wengi wa abiria walikuwa wanafunzi waliokuwa wakirejea shuleni.

St John ilisema ajali hiyo ya siku ya Jumatano ilitokea baada ya matatu ambayo wanafunzi hao walikuwamo kugongana na lori uso kwa uso.

"Majeruhi walipokea Huduma ya Kwanza kwenye eneo na walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Naivasha," St John Ambulance ilisema.

Kisa hicho kinajiri siku moja baada ya watu 15 kufariki katika ajali iliyotokea katika Barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Ajali hiyo ilihusisha basi na matatu ya abiria 14. Wahanga hao ni pamoja na watu wazima wanane na watoto saba wakiwemo wasichana watano.

Kulingana na polisi, wengine 38 walinusurika bila majeraha katika ajali hiyo.

Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia zaidi ya 20 katika ajali tofauti ndani ya siku mbili, kama ilivyoripotiwa na polisi.

Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa tisa kasorobo asubuhi katika eneo la Twin Bridge, na ilihusisha mgongano kati ya basi na matatu.

Polisi walithibitisha kuwa watu wote waliokuwa kwenye matatu hiyo walipoteza maisha

Abiria watatu wa basi walipata majeraha mabaya, huku wengine kumi wakipata majeraha madogo.

Polisi kutoka Mau Summit walijibu mara moja, na kusaidia kuwahamisha majeruhi hao hadi Hospitali ya Molo.

Mkuu wa polisi wa Bonde la Ufa Tom Odero alitoa wito kwa madereva wote kuwa waangalifu sana barabarani ili kuzuia ajali za barabarani.