Mbunge Salasya akamatwa kwa madai ya kumshambulia MCA kwenye mazishi

Aliachiliwa Ijumaa jioni kwa dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu akisubiri kufikishwa mahakamani Jumanne.

Muhtasari

•Salasya alikamatwa Ijumaa na kuachiliwa kwa dhamana kufuatia madai ya kumshambulia MCA wakati wa mazishi katika eneo la Mumias.

•Mlalamisjhi alidai alimkaribisha Salasya jukwaani na kumwomba mbunge huyo kudumisha adabu katika hotuba yake.

MBUNGE PETER SALASYA
Image: HISANI

Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Kalerwa Salasya alikamatwa Ijumaa na kuachiliwa kwa dhamana kufuatia madai ya kumshambulia mjumbe wa bunge la kaunti ya Kakamega wakati wa mazishi katika eneo la Mumias.

Mwanasiasa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumanne, Januari 16, akikabiliwa na mashtaka ya kushambulia, kudhuru mwili na kuvuruga amani.

Kisa hicho kilijiri wakati Salasya alipohudhuria mazishi ya Jesmus Kodia katika kijiji cha Maraba.

Kulingana na anayedaiwa kuwa mwathiriwa, MCA Peter Walunya Indimuli, alimkaribisha Salasya jukwaani na kumwomba mbunge huyo kudumisha adabu katika hotuba yake.

Hii inasemekana ilisababisha Salasya kumzomea Indimuli na kumwamuru aketi; hatimaye kusababisha mapambano ya kimwili ambapo alimzaba kofi.

Zogo hilo lilizua taharuki miongoni mwa waombolezaji, huku hali hiyo ikiongezeka huku milio ya risasi zikisikika. Maafisa waliingilia kati, na polisi kutoka Shianda walifika kurejesha utulivu na kuruhusu mazishi kuendelea.

Indimuli alipiga ripoti kwa polisi na kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu, na kusababisha kukamatwa kwa Salasya.

Tukio hili linaongeza utata unaomzunguka mbunge huyo wa muhula wa kwanza. Kwa sasa anachunguzwa kwa madai ya kumtishia hakimu katika kesi tofauti, huku faili ya polisi ikihakikiwa.

Salasya bado hajatoa maoni yake hadharani kuhusu madai ya kushambuliwa hivi majuzi.