Mtu anayechukua mambo ya tohara kama kitu kubwa sana ni mpumbavu- Raila Odinga

Raila alidai kuwa tohara ni utaratibu wa kimila ambao unafanywa na Wabantu wa Kenya pekee.

Muhtasari

•Raila alidai kuwa tohara ni utaratibu wa kimila ambao unafanywa na Wabantu wa Kenya pekee na haifanywi na Wabantu katika mataifa mengine.

•Raila alidai kuwa tohara ni suala dogo sana na akakashifu wale wanaochukulia mila hiyo kwa uzito huku akiwaita wapumbavu.

Raila Odinga
Raila Odinga Raila Odinga
Image: HISANI

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amekashifu kitendo cha kubaguliwa kwa wanaume ambao hawajatahiriwa.

Wakati akizungumza mjini Busia katika ziara yake inayoendelea katika eneo la Magharibi, mgombea huyo wa urais katika uchaguzi wa 2022 alibainisha kuwa kuwadhalilisha baadhi ya wanaume kwa sababu hawajatahiriwa ni upumbavu.

Raila alidai kuwa tohara ni utaratibu wa kimila ambao unafanywa na Wabantu wa Kenya pekee na haifanywi na Wabantu katika mataifa mengine.

‘Kama hapa Uganda, ni makabila mawili ambayo yanatahiri, Wagishu ambao wanahusiana na Wabukusu, na Wabakojo ambao wako kule kwa mlima peke yake. Waganda, Basoga, Wanyankole, Wabanyoro,Wabatoro, Wateso, Wachori wote hawatahiri,” Raila alisema.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alisema kuwa tohara ni mila ya kidini iliyoanzishwa na wageni walioleta dini barani Afrika.

“Hii mambo ya tohara ni ya Wabantu wa Kenya pekee yake. Bantu pande ile hawatahiri. Hii mambo ya tohara ni kitu cha dini tu. Ilikuja na dini ambayo ilipita huko Ethiopia na ikaingia hapa Kenya kwa Wabantu,” alisema.

Aliongeza, “Wabaantu ukiingia pale DRC hawatahiri. Hata ukienda pale Cameroon hawatahiri. Ata ukienda kule Afrika Kusini hawatahiri.”

Raila alidai kuwa tohara ni suala dogo sana na akakashifu wale wanaochukulia mila hiyo kwa uzito huku akiwaita wapumbavu.

“Hii mambo ya tohara ni kidogo sana. Mtu ambaye anachukua mambo ya tohara kama ni kitu kikubwa sana ni mpumbavu. Mpumbavu sana,” alisema.

Pia alikashifu mila ya ukeketaji wa wanawake akisema si jambo la kujivunia.

“Kama ile mambo ya kutahiri kina mama. Unaenda kukata kinembe cha kina mama. Alafu anafikiria amefanya kazi muhimu, ni ujinga huo,’ alisema.

Kiongozi huyo wa muungano wa Azimio la Umoja alitoa maoni hayo wakati akikashifu ubaguzi wa baadhi ya jamii za Magharibi mwa Kenya kuhusu suala la tohara.