Mwanamume akamatwa kwa mauaji ya mwanamke Narok, vitu vyenye damu vyapatikana

Maafisa waliweza kupata vitu kadhaa vilivyokuwa na damu ikiwa ni pamoja na jozi ya buti, kifyekeo na mtaimbo.

Muhtasari

•Mshukiwa ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumuua mwanamke mwenye umri wa miaka 45 katika eneo ndogo la Kilae, eneo la Moyoi, kaunti ya Narok.

•Mwili wa marehemu ulikuwa na michirizi kwenye mkono wa kulia kwenye kiwiko cha mkono, tumboni na mguu wa kulia.

Image: NPSA

Mwanamume mwenye umri wa miaka 46 ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumuua mwanamke mwenye umri wa miaka 45 katika eneo ndogo la Kilae, eneo la Moyoi, kaunti ya Narok.

Tume ya Huduma ya Kitaifa kwa Polisi imeripoti kuwa Patrick Mujitwa ambaye anashukiwa kumuua Bi Sarah aliwekwa rumande na maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Lolgorian na maafisa wa DCI kutoka afisi ya Transmara Kusini baada ya kukamatwa awali na wananchi.

Kundi la raia wenye ghadhabu walimkamata mshukiwa kufuatia kitendo hicho cha kikatili na kumfunga kwa kamba kabla ya kuwaita polisi waliomtia pingu na kumpeleka kituoni huku uchunguzi zaidi ukitarajiwa kufanyika.

Polisi walipofika eneo la tukio, walikuta mwili wa mwanamke aliyeuawa ukiwa umetapakaa kwenye dimbwi la damu huku ukiwa na michirizi mingi sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani, mkono wa kulia kwenye kiwiko cha mkono, tumboni na mguu wa kulia.

Baada ya kuchunguza boma la mshukiwa, maafisa waliweza kupata vitu kadhaa vilivyokuwa na damu ikiwa ni pamoja na jozi ya buti, kifyekeo na mtaimbo.

Kisha mshukiwa alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Lolgorian akisubiri kufikishwa mahakamani huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo uking’oa nanga.

Kwa upande mwingine, mwili wa marehemu Sarah ulipelekwa katika Hospitali ya Lolgorian Level IV ukisubiri uchunguzi wa maiti.