Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kabarak auawa kwa kuchomwa kisu karibu na shule

Marehemu alikuwa na jeraha kubwa la kudungwa tumboni kutumia silaha yenye ncha kali.

Muhtasari

•Marehemu alipatikana na majeraha ya visu kando ya barabara ya Nakuru-Mogotio karibu na kituo cha biashara cha Kampi Ya Moto, polisi walisema.

•Polisi walitembelea hospitali na eneo la tukio kama sehemu ya uchunguzi wa mauaji hayo.

Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Maafisa wa upelelezi wanachunguza kisa ambapo mwanafunzi wa shule ya uuguzi katika Chuo Kikuu cha Kabarak mjini Nakuru alipatikana amefariki barabarani Ijumaa asubuhi.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu ,Derrick Malumasa Sabuni, 23, alipatikana na majeraha ya visu kando ya barabara ya Nakuru-Mogotio karibu na kituo cha biashara cha Kampi Ya Moto, polisi walisema.

Wenzake katika chuo kikuu waliambia polisi walimpata barabarani, wakamchukua na kumkimbiza katika kituo cha afya cha Chuo Kikuu cha Kabarak ambapo alitangazwa kuwa amefariki.

Marehemu alikuwa na jeraha kubwa la kudungwa tumboni kutumia silaha yenye ncha kali na watu wasiojulikana, polisi walisema.

Maafisa wa upelelezi wanashuku kuwa mwathiriwa alidungwa kisu wakati wa tukio la wizi usiku wa manane. Vitu vyake havikuwepo katika eneo la tukio.

Polisi walitembelea hospitali na eneo la tukio kama sehemu ya uchunguzi wa mauaji hayo.

Sababu ya mauaji hayo bado haijajulikana.

Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Annex cha Manispaa ya Nakuru ukisubiri uchunguzi wa maiti na uchunguzi zaidi.

Hakuna aliyekamatwa hadi sasa.

Wapelelezi walitarajiwa kurejea eneo la tukio Ijumaa kama sehemu ya uchunguzi wa mauaji hayo.