Ajali mbaya yaua watu watatu katika Barabara kuu ya Webuye-Malaba

Tukio hilo la kutisha lilihusisha trela ambazo zilikuwa zikienda pande kinyume.

Muhtasari

•Wakaazi waliozungumza na Wanahabari katika eneo la ajali siku ya Jumapili walisema trela hizo zilikuwa zikisafirisha mahindi na saruji mtawalia.

•Wenyeji walitoa wito kwa mamlaka husika kuweka matuta kwenye barabara kuu ya Webuye-Malaba yenye shughuli nyingi.

Eneo la tukio ambapo ajali hiyo mbaya ilitokea Januari,28,2024.
Image: TONY WAFULA

Madereva wawili wa lori na mtu mmoja anayeaminika kuwa msaidizi wake walifariki papo hapo kwenye ajali iliyotokea saa tatu asubuhi siku ya Jumapili

Tukio hilo la kutisha lilihusisha trela ambazo zilikuwa zikienda pande kinyume.

Wakaazi waliozungumza na Wanahabari katika eneo la ajali siku ya Jumapili walisema trela hizo zilikuwa zikisafirisha mahindi na saruji mtawalia.

Geoffrey Wasike, mkazi, alisema kwamba alisikia mlipuko mwendo wa saa tatu asubuhi Jumapili.

"Nilikuwa bado nimelala niliposikia mlipuko barabarani, niliamka kujua kinachoendelea," Wasike alisema.

"Nilipofika eneo la ajali nilikuta miili mitatu ikiwa kwenye dimbwi la damu huku mtu mmoja akiwa amepoteza fahamu."

Aliripoti kuwa watatu hao walijeruhiwa kiasi cha kutotambulika.

Wasike alisema kuwa aliyepoteza fahamu alikimbizwa katika hospitali moja katika mji wa Bungoma kwa matibabu ya haraka huku waliofariki wakichukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Bungoma kwa ajili ya kuhifadhiwa wakisubiri wanafamilia kutambuliwa.

Wenyeji walitoa wito kwa mamlaka husika kuweka matuta kwenye barabara kuu ya Webuye-Malaba yenye shughuli nyingi.

Juhudi za kupata maoni ya polisi kuhusu tukio hilo hazikufua dafu hadi wakati wa kuchapishwa.