Polisi auawa kwa risasi baada ya kambi ya Elgeyo Marakwet kuvamiwa

Wenzake wengine wawili waliokuwa kwenye kambi hiyo walitoroka bila majeraha.

Muhtasari

•Sajenti Anthony Mwangi alipigwa risasi kichwani alipokuwa akienda kwenye choo cha nje mwendo wa saa kumi asubuhi.

•Polisi walisema kuwa genge hilo lilikuwa likilipiza kisasi mauaji ya mshukiwa wa ujambazi kwa jina Oliver Kimutai almaarufu Mutee.

Image: HISANI

Afisa mmoja wa polisi alipigwa risasi na kuuawa katika uvamizi mbaya kwenye kambi moja katika eneo la Chesuman, Elgeyo Marakwet.

Uvamizi huo ulifanyika Jumamosi, Februari 10 asubuhi katika kambi ya chifu wa Chepkum, polisi walisema.

Sajenti Anthony Mwangi alipigwa risasi kichwani alipokuwa akienda kwenye choo cha nje mwendo wa saa kumi asubuhi, polisi walisema.

Wenzake wengine wawili waliokuwa kwenye kambi hiyo walitoroka bila majeraha.

Polisi walisema idadi isiyojulikana ya watu wenye silaha walivamia kambi hiyo kwa lengo la kulipiza kisasi.

Polisi walisema kuwa genge hilo lilikuwa likilipiza kisasi mauaji ya mshukiwa wa ujambazi kwa jina Oliver Kimutai almaarufu Mutee aliyekuwa akiyesakwa .

Timu zaidi za usalama zilitumwa katika eneo hilo kufuatilia genge hilo huku kukiwa na wasiwasi kwamba hali ilikuwa ngumu kudhibitiwa.

Zaidi ya watu 20 wameuawa katika mashambulizi tofauti katika eneo hilo katika miezi kadhaa iliyopita huku kukiwa na wito wa kushughulikia tishio la ujambazi.

Haya yanajiri huku kukiwa na oparesheni endelevu za timu za mashirika mbalimbali dhidi ya matukio hayo.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amekuwa shughuli akiongoza shughuli katika eneo hilo akiapa kumaliza tishio hilo.

Kindiki alisema wizi wa ng'ombe Kaskazini mwa Kenya kwa miaka mingi umekuwa ukifanywa na shirika la uhalifu lililopangwa linalohusika na mauaji, umaskini na kufurushwa.

"Athari zake ni kali. Inazinyima jamii za wafugaji tegemeo lao la kiuchumi na kuzidisha hali ya umaskini katika nyanda za malisho, na kuchochea malalamiko ya jamii na mashambulizi ya kulipiza kisasi,” alisema.

Ili kubomoa miundombinu ya wezi wa mifugo na wawezeshaji alisema, serikali inaendeleza vita dhidi ya ujambazi na wahusika, wawezeshaji, wafadhili na wanufaika kwa kufanya ujambazi kuwa jambo chungu, kuhakikisha urejeshaji wa mifugo iliyoibiwa na kuwazawadia wawezeshaji wa urejeshaji.