Rais wa Hungary ajiuzulu kwa kutoa msamaha katika kesi ya unyanyasaji wa watoto kingono

Bi Katalin Novak alijiuzulu kutoka wadhifa wake wa urais wa Hungary katika kipindi cha moja kwa moja kwenye televisheni.

Muhtasari

•Rais Katalin Novak kumsamehe mtu ambaye alikuwa amepatikana na hatia ya kuficha kesi ya unyanyasaji wa watoto kingono.

•Judit Varga, waziri wa zamani wa sheria aliyeidhinisha msamaha huo, pia amejiuzulu nafasi yake mpya .

Image: TWITTER// KATALIN NOVAK

Rais wa Hungary, Bi Katalin Novak mnamo Jumamosi jioni alijiuzulu kutoka wadhifa wake kupitia kipindi cha moja kwa moja kwenye televisheni kufuatia uamuzi wake wa kumsamehe mtu ambaye alikuwa amepatikana na hatia ya kuficha kesi ya unyanyasaji wa watoto kingono.

Uamuzi wa Kovak kujiuzulu ulifuatia maandamano ya raia wa nchi hiyo ya Ulaya kuhusu uamuzi wake wa kumsamehe afisa ambaye alikuwa amefungwa jela kwa kuwalazimisha watoto kufuta madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mkurugenzi wa makao ya watoto yanayosimamiwa na serikali.

Wakati akitoa hotuba yake moja kwa moja kwenye televisheni siku ya Jumamosi, rais huyo wa kike alisema alitoa msamaha huo kwa imani kuwa mwanamume aliyehukumiwa hakutumia vibaya udhaifu wa watoto waliokuwa chini ya uangalizi wake. Alikubali kosa lake na akaomba radhi kwa kutoa msamaha huo.

"Nilifanya makosa, kwani msamaha na ukosefu wa hoja ulisaidia kuzua mashaka juu ya kutostahimili sifuri ambayo inatumika kwa wanyanyasaji wa watoto," Novak alisema.

Mzozo uliosababisha kujiuzulu ulikuja baada ya majina ya watu 25 waliosamehewa na Novak mwezi Aprili mwaka jana, kama sehemu ya ziara ya Papa Francis nchini Hungary, kuwekwa hadharani na vyombo vya habari vya Hungary wiki iliyopita.

Katika orodha ya wafungwa kulikuwa na naibu mkurugenzi wa makao ya watoto karibu na Budapest, ambaye alikuwa amefungwa kwa miaka mitatu baada ya kuwalazimisha watoto kufuta madai ya unyanyasaji dhidi ya mkurugenzi wa nyumba hiyo. Mkurugenzi huyo alikuwa amefungwa jela kwa miaka minane kwa kosa la kuwadhulumu watoto katika kituo hicho kinachosimamiwa na serikali.

Vyama vya upinzani vya Hungary na waandamanaji walikuwa wakimtaka ajiuzulu, lakini uamuzi wa Novak kufanya hivyo ulikuwa wa ghafla kama vile haukutarajiwa.

"Leo nimejiuzulu kutoka ofisi yangu kama Rais wa Hungary. Asante kwa kila kitu marafiki zangu wote katika pembe zote nne za dunia.

Hungaria ni nchi nzuri yenye watu wazuri, mshirika mzuri, rafiki bora na mshirika anayetegemeka. Nina furaha kwamba katika miaka iliyopita ningeweza kufanya kazi ili kuhamasisha watu kuhusu hili duniani,” Novak alisema kupitia Twitter.

Judit Varga, waziri wa zamani wa sheria aliyeidhinisha msamaha huo, pia amejiuzulu nafasi yake mpya ya kuongoza kampeni za uchaguzi wa Ulaya kwa chama tawala cha Waziri Mkuu Viktor Orban cha Fidesz.

Novak alikua mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa mkubwa wa urais wa Hungary mnamo mwaka wa 2022.