Drama huku mwanamke akikatiza hotuba ya Ruto wakati wa mazishi ya Kelvin Kiptum

Hili lilimlazimu Rais kusitisha hotuba yake ili kuingilia kati.

Muhtasari

•Mwanamke huyo ambaye bado hajajulikana alizua taharuki wakati tu Rais William Ruto alipokuwa akitoa hotuba yake.

•Rais alijaribu kuwaambia walinzi wamuache na kumruhusu aketi.

Picha ya mwanamke aliyekatiza hotuba ya Rais William Ruto
Picha ya mwanamke aliyekatiza hotuba ya Rais William Ruto
Image: HISANI

Kulikuwa na drama wakati wa mazishi ya mwanariadha wa mbio za marathoni Kelvin Kiptum baada ya mwanamke kusababisha usumbufu.

Mwanamke huyo ambaye bado hajajulikana alizua taharuki wakati tu Rais William Ruto alipokuwa akitoa hotuba yake.

Hili lilimlazimu Rais kusitisha hotuba yake ili kuingilia kati.

Katika video hiyo, mwanamke huyo, ambaye huenda alijaribu kumfikia Rais alizuiliwa na walinzi na kufukuzwa.

Rais alijaribu kuwaambia wamuache na kumruhusu aketi.

"Achana naye, muache akae tu hapa, mpeleke akae hapa, akae pale" Rais alisema huku akionyesha sehemu anayoipendelea zaidi ambapo alimtaka mwanamke huyo aketi.

Mwanamke huyo hata hivyo alionekana kuwazidi nguvu maafisa wawili waliokuwa wakimuelekeza kulingana na agizo la Rais.

Hii iliwalazimu maafisa zaidi kuingia na kumpeleka nyuma ya hema.

Haijulikani nia yake ilikuwa nini au nini kilifanyika baadaye.