Kenya yaondoa ada ya kuingia nchini kwa Waafrika Kusini na mataifa kadhaa ya kigeni

Serikali ilitupilia mbali mahitaji ya viza kwa wamiliki wote wa pasipoti za kigeni mwezi uliopita.

Muhtasari

•Hatua hiyo ilionekana kama jaribio la kuitangaza Kenya kama kivutio cha utalii na kuvutia wasafiri wa kibiashara.

•San Marino, taifa la tatu kwa udogo barani Ulaya, ndiyo nchi nyingine pekee kwenye orodha ya kutotozwa ada.

Image: BBC

Kenya imewaondolea ada ya kuingia nchini wamiliki wa pasipoti za kusafiria kutoka Afrika Kusini na nchi nyingine sita bada ya ada hiyo kuanzishwa mwezi uliopita .

Serikali ilitupilia mbali mahitaji ya viza kwa wamiliki wote wa pasipoti za kigeni mwezi uliopita.

Hatua hiyo ilionekana kama jaribio la kuitangaza Kenya kama kivutio cha utalii na kuvutia wasafiri wa kibiashara.

Lakini ada ya kuingia ya $30 (£23) ilianzishwa, ikijumuisha kwa baadhi ya wageni ambao hapo awali hawakuhitaji visa.

Uamuzi huo ulizua msukosuko mkubwa, huku wakosoaji wakisema kuwa huenda ukasababisha nchi ambazo Kenya ina mikataba ya kuondoa viza kuanzisha ada sawa na hiyo, hivyo kufanya usafiri kuwa wa gharama kubwa .

Ni wasafiri tu kutoka jumuiya ya kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao hawakuruhusiwa kulipa pesa hizo.

Mbali na Afrika Kusini, msamaha huo umeongezwa kwa wamiliki wa pasipoti kutoka mataifa mengine matano ya Afrika - Ethiopia, Eritrea, Congo-Brazzaville, Comoro na Msumbiji.

San Marino, taifa la tatu kwa udogo barani Ulaya, ndiyo nchi nyingine pekee kwenye orodha ya kutotozwa ada.

Taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya ndani ya Kenya na idara ya uhamiaji ilisema nchi zisizohitajika kulipa ada hiyo zimeingia "mkataba wa kukomesha visa au kutia saini makubaliano ya pande mbili ya kuondoa visa" na taifa hilo la Afrika Mashariki.

Hata hivyo, wasafiri kutoka nchi hizi bado watahitaji kupata hati ya uidhinishaji wa usafiri wa kielektroniki (ETA) mapema ili kuingia Kenya, na kuwasilisha maelezo kama vile maelezo ya ndege na uthibitisho wa mahali pa kulala.

ETA ni idhini ya kuingia mara moja nchini na ni halali kwa siku 90.