Wanafunzi kadha wahofiwa kufa baada ya basi la shule kupinduka Murang'a

Uchunguzi umeanzishwa na polisi kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Muhtasari
  • Kulingana na ripoti, wanafunzi wawili wanadaiwa kuaga dunia wakipokea matibabu katika hospitali ya Murang'a Level 5.

Wanafunzi kadhaa walihofiwa kufariki Jumamosi baada ya basi la Shule ya Msingi ya Maadili kupinduka eneo la Mathioya, Murang'a.

Kulingana na ripoti, wanafunzi wawili wanadaiwa kuaga dunia wakipokea matibabu katika hospitali ya Murang'a Level 5.

Walioshuhudia ajali hiyo walieleza kuwa wanafunzi hao walikuwa wakitoka kwenye hafla ya skauti katika Kaunti ya Nyeri ajali hiyo ilipotokea.

Waliongeza kuwa basi la shule lilipoteza udhibiti na kuacha barabara kabla ya kupinduka katika kichaka kilicho karibu.

Idadi kamili ya vifo na majeruhi bado haijajulikana.

Maafisa wa polisi walifika eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali hiyo huku shughuli za uokoaji zikianzishwa kuokoa wanafunzi zaidi waliokuwa wamekwama ndani ya mabaki ya basi.

Katika picha zilizosambazwa kwa wingi, basi hilo lilikuwa limeharibika kabisa huku vioo vyake vikiwa vimevunjwa na kutapakaa kila mahali, ikionyesha ukubwa wa ajali hiyo.

Uchunguzi umeanzishwa na polisi kubaini chanzo cha ajali hiyo.