Nyoya Raila ya AUC yang’aa, baraza kuu la AU laamua kwa kauli moja Afrika Mashariki kutoa mwenyekiti

Mudavadi, alishawishi kupitishwa kwa uamuzi huo wakati wa kikao hicho, alisema uamuzi huo unalingana na kile ambacho Kenya imekuwa ikishinikiza.

Muhtasari

 • "Sasa ni wazi kwamba Raila Odinga atakuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwa Mwenyekiti wa Tume ya AU,"  Mudavadi alisema. 

Makao makuu ya umoja wa Afrika mjini Addis Ababa
Makao makuu ya umoja wa Afrika mjini Addis Ababa

Baraza Kuu la Umoja wa Afrika limekubaliana kwa kauli moja kuwa ni zamu ya kanda ya Afrika Mashariki kutoa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Afrika (AUC). 

Uamuzi huo ulitolewa siku ya Ijumaa wakati wa Kikao cha 22 maalum cha Halmashauri Kuu ya AU. Uamuzi huo ni kwa mujibu wa Mkataba wa baraza la AU, Kanuni za Uendeshaji wa vyombo vya sera za Umoja wa Afrika na maamuzi ya Bunge la Wakuu wa Nchi na Serikali.

 "Haya ni mafanikio makubwa kwa kanda ya Afrika Mashariki kuwasilisha wagombeaji wa nafasi ya Mwenyekiti wa AUC," Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi alisema. 

Mudavadi, ambaye alishawishi kwa dhati kupitishwa kwa uamuzi huo wakati wa kikao hicho, alisema uamuzi huo unalingana na kile ambacho Kenya imekuwa ikishinikiza. 

"Sasa ni wazi kwamba Raila Odinga atakuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwa Mwenyekiti wa Tume ya AU," alisema. 

"Kwa kweli, hakuna vikwazo vya kiufundi au kisheria vinavyozuia Kenya kuwasilisha mgombea wake." 

Nafasi ya mwenyekiti wa AUC inatazamiwa kuwa wazi mwaka ujao, huku anayeshikilia nafasi hiyo, Moussa Faki wa Chad, akihitimisha muda wake wa mihula miwili.

Uchaguzi utafanyika Februari 2025. Uamuzi huo pia unatoa kwamba kanda ya Kaskazini mwa Afrika itachuana na wagombea wa Naibu Mwenyekiti wakati maeneo mengine matatu, Kati, Kusini na Magharibi, yakiwania nafasi sita za makamishna. 

Katika taarifa, Mudavadi alisema Kenya itafanya kazi kwa karibu ndani ya mataifa 14 wanachama wa ukanda wa Afrika Mashariki ili kujenga mwafaka kuhusu mgombea wake.

 "Juhudi hizi zinaendelea na zitaendelea, kujumuisha maeneo mengine yote ili kuhakikisha kuwa fursa ya kuchagua uongozi bora wa AUC inatoa jukwaa la kuunganisha bara zima," aliongeza. 

Kinara wa upinzani Raila Odinga ametangaza rasmi kuwania kiti hicho na hivyo kuweka mazingira mazuri ya kuwania uongozi wa kihistoria.Raila alitangaza kuwa tayari kugombea nafasi hiyo yenye ushawishi mkubwa, akiangazia mashauriano yake ya kina na washirika kabla ya kufanya uamuzi huo. 

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, anayemuunga mkono Raila kuwania kiti hicho, amesisitiza umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Afrika Mashariki kutwaa uenyekiti wa AUC.