Apofuka baada ya kutumia mkojo kutibu ugonjwa wa macho

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa ameambukizwa ugonjwa wa macho mapema mwezi huu.

Muhtasari

• "Niliosha macho yangu kwa sabuni na mkojo," alisema. Bw Aiuba alisema haya ni "mazoea ya watu katika eneo hili".

Image: BBC

Mwanamume mmoja nchini Msumbiji amepofuka baada ya kutumia dawa za kienyeji na mkojo kutibu ugonjwa wa macho.

Babu Aiuba kwa sasa anapata matibabu katika Hospitali Kuu ya Quelimane.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa ameambukizwa ugonjwa wa macho mapema mwezi huu.

"Niliosha macho yangu kwa sabuni na mkojo," alisema. Bw Aiuba alisema haya ni "mazoea ya watu katika eneo hili".

Lakini hii ilifanya jicho lake kuwa baya zaidi. Hatimaye alipoteza uwezo wa kuona. Daktari wa macho Eugénia Cavele alisema utumiaji wa dawa za kienyeji ulifanya ugonjwa kuendelea hadi upofu.

"Ningependa kuonya kila mtu ambaye ana dalili za ugonjwa huu kutotumia vitu ambavyo havijathibitishwa kisayansi na kutojitibu, kwani hii inaweza kusababisha upofu," Bw Cavele alisema.

Hiki ni kisa cha kwanza cha upofu unaosababishwa na matibabu ya jadi tangu ugonjwa kuzuka Msumbiji.

Ugonjwa huu unaathiri karibu majimbo yote ya Msumbiji, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Maputo.

Mamlaka pia zimeripoti kesi za ugonjwa huo kwenye jengo la Magereza la Mkoa wa Maputo.

Takribani wafungwa 270 wa gereza hilo wameambukizwa. Mlipuko wa ugonjwa wa macho umekumba nchi nyingine kadhaa mashariki na kusini mwa Afrika.