Kijana wa miaka 22 afariki kwa kujitoa uhai baada ya kuzozana na mama yake

Marehemu alipopekuliwa mfukoni mwake alikuwa ameacha barua ya kujitoa uhai.

Muhtasari

•Kisa hicho kilitokea Ijumaa katika Kaunti ya Samburu na kuripotiwa katika kituo cha polisi cha Maralal.

•"Hakuna kitu nilichofanya kukufanya unichukie hivi, si vibaya kumuadhibu mtu namna hii, lakini ni mbaya kumuadhibu mtu kwa jambo ambalo hajafanya," ilisomeka barua hiyo.

Kitanzi
Kitanzi
Image: HISANI

Mwanamume mwenye umri wa miaka 22 amefariki kwa kujitoa uhai kufuatia uhusiano mbaya na mamake.

Kisa hicho kilitokea Ijumaa katika Kaunti ya Samburu na kuripotiwa katika kituo cha polisi cha Maralal.

"Takriban saa sita mchana mwili wa mwanamume mmoja wa Samburu wa umri wa makamo ulipatikana ukining'inia kwenye mti karibu na boma lao lpartuk," ripoti ya OB ya polisi ilisoma kwa sehemu.

Kulingana na polisi, kijana huyo muda alifariki kwa kujitoa uhai katika muda usiojulikana.

Kisa hicho kiliripotiwa na Mark Loloolki ambaye ni mkazi wa kijiji cha lpartuk ndani ya eneo la Maralal.

Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Maralal na DCI Samburu Central walitembelea eneo la tukio.

Hapo ndipo ilipothibitishwa kuwa marehemu alipopekuliwa mfukoni mwake alikuwa ameacha barua ya kujitoa uhai.

Eneo la tukio lilishughulikiwa na kurekodiwa huku mwili ambao haukuwa na majeraha yoyote yaliyoonekana ukiondolewa na kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya kaunti ya Samburu ikisubiri uchunguzi wa maiti.

Katika barua hiyo ya kujitoa uhai, marehemu aliielekeza kwa mama yake.

Alisema alimsikia akimwambia mtu wa tatu kwamba alikuwa amechoshwa naye.

"Hakuna kitu nilichofanya kukufanya unichukie hivi, si vibaya kumuadhibu mtu namna hii, lakini ni mbaya kumuadhibu mtu kwa jambo ambalo hajafanya," ilisomeka barua hiyo.

"Leo ni siku yangu ya mwisho ya kuteseka, lakini natumai hautatoa chozi kwa ajili yangu kwa sababu wote waliniona kama mnyama bure."