Watembea kwa miguu wakamatwa kwa kutotumia madaraja ya miguu jijini Nairobi

"Asubuhi ya leo, watembea kwa miguu kadhaa ambao walikosa kutii sheria za trafiki walizuiliwa.

Muhtasari
  • Kupitia kwenye ukurasa rasmi wa  X NTSA ilisema kuwa ni sharti watembea kwa miguu watumie njia zilizowekwa na maeneo ya kupita ili kuwahakikishia usalama.
Image: NTSA/X

Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) imewatia mbaroni watembea kwa miguu kadhaa kwa kukosa kutumia njia na madaraja ya watembea kwa miguu wakati wakivuka barabara katika mji mkuu.

Kupitia kwenye ukurasa rasmi wa  X NTSA ilisema kuwa ni sharti watembea kwa miguu watumie njia zilizowekwa na maeneo ya kupita ili kuwahakikishia usalama.

"Ni lazima watembea kwa miguu watumie madaraja ya miguu yanayopatikana, njia za kupita na sehemu nyingine zilizoteuliwa ili kuhakikisha usalama wao."

Iliongeza;

"Asubuhi ya leo, watembea kwa miguu kadhaa ambao walikosa kutii sheria za trafiki walizuiliwa.

Ili kuepusha usumbufu wowote, tunawahimiza watembea kwa miguu kuzingatia sheria za trafiki."

Picha zilizoshirikiwa na Mamlaka zinaonyesha maafisa wa NTSA pamoja na maafisa wa polisi wakiwakamata watembea kwa miguu katika maeneo tofauti ya vivuko katika mji mkuu.

Msako huo unakuja kama sehemu ya mageuzi mapya yaliyoanzishwa katika sekta hiyo na Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki kufuatia kuongezeka kwa ajali.

Operesheni hiyo iliyoanzishwa mwanzoni mwa Machi, ambayo awali iliwalenga madereva, ilisababisha kukamatwa kwa madereva 22,958, kati yao 1,086 wakikabiliwa na mashtaka ya kuendesha gari wakiwa walevi.

Kulingana na takwimu za ajali kutoka NTSA, watembea kwa miguu pia wanachangia vifo vingi pamoja na waendesha pikipiki na abiria pamoja na abiria wa magari ya huduma ya umma.