Watu wawili wafariki , 10 wajeruhiwa baada ya basi kugonga lori la mafuta Kikuyu

Basi la abiria 32 liligonga lori la mafuta lililokuwa limekwama barabarani mwendo wa saa kumi na moja unusu asubuhi.

Muhtasari

•Miili ya abiria hao wawili ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Thogoto, huku mabaki ya magari hayo yakivutwa hadi Kituo cha Polisi cha Kikuyu.

•Polisi pia walifichua kuwa zaidi ya abiria 10 waliopata majeraha mabaya walikimbizwa katika hospitali ya Kikuyu ambako wanapokea matibabu.

liligonga lori la mafuta huko Kikuyu mnamo Aprili 6, 2024.
Basi lililokuwa likitoka Magharibi kuelekea Nairobi liligonga lori la mafuta huko Kikuyu mnamo Aprili 6, 2024.
Image: HISANI

Watu wawili walifariki Jumamosi asubuhi na wengine 10 kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani.

Polisi walilaumu uonekano mbaya miongoni mwa sababu zingine wakati wa ajali hiyo ilitokea eneo la Muguga, Kikuyu, Kaunti ya Kiambu.

Kamanda wa Polisi wa Kikuyu Ronald Kirui alisema basi hilo la abiria 62 la Kampuni ya Eldoret Express liligonga lori la mafuta lililokuwa limekwama barabarani mwendo wa saa kumi na moja unusu asubuhi.

"Tulipata vifo viwili na zaidi ya kumi walikimbizwa hospitalini. Eneo hilo kwa sasa limenyesha kutokana na mvua na tunawaomba madereva kuwa makini,” alisema.

Polisi pia walifichua kuwa zaidi ya abiria 10 waliopata majeraha mabaya walikimbizwa katika hospitali ya Kikuyu ambako wanapokea matibabu.

Miili ya abiria hao wawili ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Thogoto, huku mabaki ya magari hayo yakivutwa hadi Kituo cha Polisi cha Kikuyu.

Kamanda wa Polisi alisema polisi wa usalama barabarani wameanzisha uchunguzi ili kubaini ni nini kilitokea na kusababisha ajali hiyo mbaya.

"Kufikia sasa hatuwezi kufahamu kilichosababisha ajali hiyo, lakini maafisa wetu wa trafiki wameanza uchunguzi," alisema.

Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari, na kuwalazimu madereva waliokuwa wakielekea Nairobi kutumia njia mbadala katika vijiji vya Muguga na kujiunga na barabara kuu ya Kinoo.

Basi hilo lilikuwa likielekea Nairobi kutoka eneo la Magharibi lilipogonga lori ya mafuta.

Simon Kimani, mkazi aliyeshuhudia ajali hiyo, alisema walivutiwa na sauti za kupasuka na kishindo kikubwa.

"Tulikimbia kuona kilichotokea na kukuta basi likiwa limegonga lori. Kwa bahati nzuri, lori hilo halikulipuka," alisema.

Kimani alisema abiria walionusurika walianza kupiga kelele za kuomba usaidizi, na wenyeji wakawaita polisi ambao walifika muda mfupi.

Watumiaji wa barabara wametakiwa kuwa waangalifu wanapotumia barabara hiyo hasa nyakati za mvua.

Hii ni ajali ya hivi punde huku kukiwa na kampeni inayoendelea ya kukabiliana na tishio hilo.

Zaidi ya watu 1,000 wamefariki katika ajali tofauti katika muda wa miezi mitatu iliyopita nchini humo.