Maajabu! Mwanaume aliyekufa wiki chache kabla ya harusi amuoa mchumba wake kabla ya kuzikwa

Mjukuu wa marehemu ambaye alichaguliwa kumsimamia wakati wa harusi ndiye aliyemvisha pete mjane Beatrice Muthoni.

Muhtasari

•Licha ya tukio hilo la kusikitisha, familia ya marehemu Martin Gitari ilifanya uamuzi mkubwa wa kuchanganya hafla za maziko na harusi.

•Baada ya harusi, mjane alibadilisha nguo za harusi kabla ya kujumuika na waombolezaji wengine kwenye hafla ya maziko.

Image: SCREEN GRAB// CITIZEN TV

Hafla ya kipekee sana ilifanyika katika eneo la Rukenya, kaunti ya Kirinyaga siku ya Jumamosi ambapo mzee wa miaka 60 ambaye alifariki wiki chache zilizopita  baada ya kuugua kwa muda alifunga ndoa na mchumba wake kabla ya kuzikwa.

Martin Gitari alifariki mnamo Machi 16, 2024, wiki tatu tu kabla ya harusi yake iliyoratibiwa kufanyika Aprili 6, 2024 katika Kanisa la Our Lady Consolata Rukenya, katika eneo bunge la Gichugu.

Licha ya tukio hilo la kusikitisha, familia ya marehemu Martin Gitari ilifanya uamuzi mkubwa wa kuchanganya hafla za maziko na harusi.

Hafla hiyo ya harusi/mazishi ilianzia katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo mjane alimvisha pete marehemu mchumba wake kabla ya mwili kusafirishwa hadi kanisani ambapo harusi kuu lilipangwa kufanyika mwendo wa saa nne asubuhi.

Beatrice ambaye alikuwa amevalia gauni zuri jeupe la harusi alisimama mbele ya kanisa kwa ajili ya kiapo cha ndoa, huku mwili wa marehemu mumewe ukiwa kando yake.

Mjukuu aliyepewa jina kama la marehemu Gitari ambaye alikuwa amechaguliwa kusimama badala yake kwenye harusi ndiye aliyemvisha pete Bi Beatrice Muthoni kidoleni.

“Mimi sijawahi kuona kitu kama hiki, nimekuwa padre miaka minne. Hata kabla nikuwe padre sijaona. Familia ilisema na ikaomba iweze kupata mtoto mmoja wa watoto ambaye anaitwa Gitari kama babu yake aweze kumsimamia na kumvisha pete nyanya yake ambaye ni Beatrice,” Padre wa Kanisa la Katoliki la Kutus, Sammy Njoroge ambaye aliongoza hafla hiyo alisema.

Shughuli muhimu zinazofanyika katika harusi ya kawaida ikiwa ni pamoja na kukata keki bado zilifanyika hata kama hii haikuwa harusi ya kawaida.

Mjane, Beatrice alisema waliamua kuendelea na mipango ya harusi ili kutimiza ndoto yake na marehemu ya kufunga ndoa ya kanisa.

“Tulikuwa tumepanga harusi lakini Mungu akamchukua mbele. Sasa leo ilikuwa siku ya harusi na mazishi. Tulimuweka pete kwa mochari, na mimi nikawekwa yangu,” Beatrice alisema.

Baada ya hafla ya harusi hiyo ya kipekee, mjane huyo alibadilisha nguo zake za harusi kabla ya kujumuika na waombolezaji wengine kwenye hafla ya maziko iliyofanyika nyumbani kwao katika eneo la Rukenya.